VIONGOZI Wa Vyama vya Siasa nchini wametakiwa kufikisha taarifa sahihi na kwa wakati kwa wanachama wao kwa kuhamasisha wanachama wenye sifa kujitokeza na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na kushiriki zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC,) Jaji (Rufaa,) Jacobs Mwambegele wakati wa mkutano ulioikutanisha Tume hiyo ni viongozi wa vyama vya siasa 19 nchini na kusema kuwa, Lengo la kukutana na viongozi hao ni kupeana taarifa za maandalizi kwa ajili ya kuanza rasmi kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura pamoja na maandalizi ya mchakato huo ikiwemo uhakiki wa vituo vya vituo vya kuandikisha wapiga kura, ununuzi wa vifaa, uboreshaji wa majaribio na ushirikishaji elimu kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, viongozi wa dini, Asasi za kiraia pamoja na makundi mbalimbali ya vijana na wanawake.
“Tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwenu, wafikishieni taarifa wanachama na wafuasi wa Vyama vyenu taarifa zinazohusu zoezi lililopo mbele yetu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa usahihi na kwa wakati ….Pamoja na kuwahamasisha wananchi wenye sifa ya kujiandikisha kuwa wapiga kura kwa kujitokeza kwa wingi kwa tarehe ambazo tayari Tume imeziweka kwa kila kituo.” Ameeleza.
Amesema, Tume hiyo imeanza mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na rasmi uboreshaji huo utazinduliwa rasmi Julai, Mosi mwaka huu mkoani Kigoma na Waziri Mkuu Kassim
majaliwa na kueleza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 umeboreshwa zaidi kwa kutumia teknolojia ya BVR (Biometric Voter’s Registration) ya kisasa zaidi kwa kuwekwa program endishi na hiyo ni pamoja na kupunguzwa uzito kwa vifaa na kubebeka kiurahisi hali itakayorahisisha kazi kwa watendaji katika maeneo mbalimbali hususani maeneo ya vijijiji.
Aidha ameeleza kuwa Tume imekuwa na utaratibu wa kuwashirikisha wadau wa uchaguzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yake na kupitia kikao hicho Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa nakala ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji kupitia Wakala mmoja kwa kila Chama ambao watashiriki kuwatambua sifa za kuandikishwa au kutoandikishwa kwa raia watakafika katika vituo hivyo.
“Niwaombe viongozi wa vyama vya siasa kwa umoja wenu tuzingatie sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya Tume kuhusu zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Tume kwa upande wetu tutazingatia kanuni, sheria ya uchaguzi kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi hili muhimu la uboreshaji.” Amefafanua.
Akitoa Mada kuhusiana na Maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima amesema, idadi ya vituo vya 40,126 vya kujiandikisha wapiga kura vitatumika katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/2025 huku vituo 39,709 vikiwa Tanzania Bara na vituo 417 vikiwa Zanzibar na kufafanua kuwa kuna ongezeko la vituo 2312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika 2019/2020.
“Tunataraji daftari litakuwa na wapiga kura 34,746,638 na idadi inaweza kuongezeka zaidi huku idadi ya wapiga kura 594, 494 itaondolewa kwa kupoteza sifa ya kuwa wapiga kura kutokana na sababu mbalimbali.” Ameongeza
Kailima amesema, kwa mujibu wa kanuni 15 (2) (c) za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Tume imeweka utaratibu wa kuandikisha wanafunzi waliopo vyuoni, magereza, mahabusu na wafungwa ambao wamehukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita na kujiandikisha kuwa wapiga kura.
Pia vifaa zikiwemo BVR 6000 pamoja na vishkwambi vitakavyotukika kuchukulia taarifa za wapiga kura, picha na saini vimenunuliwa huku BVR hizo zikiwa na mfumo endeshi wa Android zikiwa na kilogram 18 ukilinganisha na BVR za awali zilizokuwa na mfumo wa Windows na Kilogram 35.
“Maboresho makubwa ya kiteknolojia yamefanyika kupitia mfumo saidizi wa Online Voters Registration System ambao kupitia simu au computer wapiga kura waliojiandikisha katika daftari wanaweza kuanza mchakato wa kubadili taarifa za kuhama Mkoa au Wilaya kwa sharti la kuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa.” Amesema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM,) Ally Hapi ameishukuru Tume Huru ya Uchaguzi kwa kwa kushirikisha vyama vyote vya siasa katika mchakato huo muhimu katika ujenzi wa demokrasia nchini na kuwezesha zoezi la uchaguzi na kuwataka wanachama na wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili kupata haki yao ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka katika kuleta maendeleo.
Pia Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF,) Ibrahim Lipumba ameipongeza Tume hiyo kwa kuonesha utayari wa kuanza zoezi hilo kwa matumizi ya teknolojia zaidi na kulenga kuwafikia wapiga kura wapya zaidi ya milioni tano na kuwahimiza wananchi na wanachama kutumia fursa hiyo ya kupata haki yao ya msingi.
Mkutano huo umeikutanisha Tume Huru ya Uchaguzi na viongozi na wawakilishi wa Vyama 19 vya siasa nchini vikiwemo CCM, CHADEMA, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP, ACT Wazalendo, ADC, CHAUMA, Demokrasia Makini, CCK, NRA na UPDP.wenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji (Rufaa), Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mkutano wa Tume na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 07 Juni, 2024 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa DaftariMkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima, Akizungumza wakati wa mkutano wa Tume na viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo tarehe 07 Juni, 2024 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa Daftari.
0 Comments