Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA) kimelishuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kuendelea kutoa sapoti mikoani kwajili ya kukuza na kuendeleza mpira wa miguu kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa SIREFA Mkoa wa Singida, Bw. Hamisi Kitila,ametoa shukurani hizo wakati akifunga mafunzo ya awali ya ukocha wa mpira wa miguu yaliyofanyika mkoani hapa.
Alisema TFF imekuwa na msaada mkubwa katika kuhakikisha kunakuwa na walimu wazuri wa mpira wa miguu na ndio maana imekuwa ikitoa mafunzo lengo ni kuhakikisha kunakuwa na walimu ambao watafiti katika nafasi hizo.
Kitila aliwaasa makocha kwenda kutumia taaluma walioipata ili kuendeleza juhudi zinazofanywa na viongozi wetu wa kitaifa na kimataifa ilikukuza na kuendeleza michezo kwajili ya maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, Kitila amewataka makocha kushiriki vema shughuli za michezo mara kwa mara ili kuifanya taaluma walioipata kuwa hai na endelevu.
Naye Mwenyekiti wa makocha Mkoa wa Singida (TAFCA) Bw. Gabriel Gunda, aliwaomba makocha hao kujiunga kwenye Chama cha Makocha Mkoa Singida na taifa ili kuendeleza taluma na kujua mambo mengi yanayoendelea kuhusu ukocha.
Kwa upande Afisa Michezo Manispaa ya Singida,Samwel Mwaikenda aliwaasa makocha kuwa waadilifu katika kufanya kazi zao za michezo ili kuendelea kuupa thamani kubwa mchezo wa mpira wa miguu ndani na nje ya Tanzania.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida, Bw. Daudi Selemani ameahidi kuendelea kutoa ushirikisno kwa wanamichezo wote mkoani Singida ili kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza michezo ndani na nje ya nchi kwa maslahi mapana ya jamii na taifa kwa ujmla.
0 Comments