Wasomi, wanasiasa watoa neno mabadiliko serikalini.

DAR-ES-SALAAM: KUNG’OLEWA katika Baraza la Mawaziri kwa wanasiasa vijana wawili, Nape Nnauye na January Makamba kumeacha gumzo, lakini wasomi, viongozi wa siasa na wachambuzi wameeleza mabadiliko kwenye wizara yamekuwa yakilenga kuboresha utendaji wa kazi serikalini.

Nape na January waliokuwa wakiongoza wizara za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametenguliwa nyadhifa zao juzi katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan. Jerry Silaa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amemrithi Nape wakati Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo ndiye mrithi wa January.

Aidha, katika mabadiliko hayo naibu mawaziri Stephen Byabato na Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wote waliokuwa Mambo ya Nje wameondolewa, ingawa Balozi Mbarouk atapangiwa kazi nyingine wakati Byabato uteuzi wake umetenguliwa.

SOMA: Rais Samia awafuta kazi Makamba, Nape

Tangu kufanyika kwa mabadiliko hayo juzi usiku, mijadala imetawala katika mazungumzo ya kawaida mitaani na mitandaoni kuhusu kutenguliwa nyadhifa kwa wanasiasa hao wawili vijana, na taarifa ya Ikulu haikueleza sababu za kuondolewa kwao.

Wote waliwahi kuhudumu katika nafasi za uwaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli kabla ya kuwaondoa, na baadaye kuibuka katika Serikali ya Awamu ya Sita. Hata hivyo, wasomi, viongozi wa siasa na wachambuzi wamesema mabadiliko ambayo amekuwa akiyafanya mara kwa mara Rais Samia kwenye wizara yanalenga kuboresha utendaji kazi wa serikali.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema mabadiliko ambayo amekuwa akiyafanya Rais Samia katika Wizara ya Mambo ya Nje ni kwa kuwa pengine unafika wakati anaona aliyempa nafasi hajafanya kama alivyotaka kisha kulazimika kufanya mabadiliko.

Alisema Rais Samia amekuwa akiongoza kwa kufuata falsafa yake ya 4R, kwa hiyo mategemeo ni kuwa wasaidizi wake watakwenda sambamba na falsafa hizo. “Kiongozi anapozungumza maneno kama aliyozungumza Nape kule Bukoba ni kwenda kinyume na falsafa maana tulikuwa tunategemea achukuliwe hatua hata kama aliomba radhi, hata kama alisema ulikuwa utani kuna vitu haviwezi kufanyiwa utani, kama kiongozi lazima ujue mipaka,” alifafanua Dk Mbunda.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya alisema vyuo vya uongozi ni mahali sahihi pa kujua viongozi wazuri tangu wakiwa katika masomo.

Alisema Silaa alimudu vyema Wizara ya Ardhi ikiwamo kusimamia uanzishwaji wa mabaraza ya ardhi ya kata. Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Denis Konga alisema Rais anapoona utendaji unahitaji nguvu mpya na mtu atakayesimamia yale aliyopanga, ndio anaamua kufanya mabadiliko kama alivyofanya.

SOMA: https://www.trtafrika.com/sw/africa/rais-samia-awatengua-nape-na-makamba-kutoka-baraza-lake-la-mawaziri-18186439

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib na Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, alisema Balozi Kombo atamsaidia Rais kutimiza malengo yake kwani ni kiongozi mwenye uzoefu aliyeshika nafasi ya uwaziri katika Serikali ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Deogratius Ndejembi ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kabla ya uteuzi huu alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Ridhiwani Kikwete ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) akitoka kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk atakayepangiwa kituo cha kazi.

Mbunge wa Kwela, Deus Sangu ameteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mbunge wa Mikumi, Dennis Londo ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki akimbadili Byabato.

Katika uteuzi mwingine, Eliakim Maswi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo anakuwa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma kumbadili Rehema Madenge ambaye amestaafu.

Aidha, Ofisa Mwandamizi, Ofisi ya Rais Ikulu, Kiseo Nzowa ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, wakati Ofisa Mwandamizi mwingine kutoka ofisi hiyo, Musa Haji Ali ameteuliwa kuwa Balozi. Pia Louis Bura ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato akichukua nafasi ya Said Nkumba ambaye hivi karibuni alishinda Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora.

Katika uhamisho, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota amehamia Serengeti wakati Dk Vincent Mashinji amehamia Manyoni kutoka Serengeti. Dk Maulid Madeni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti huku Afraha Hassan akihamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenda kuwa DED Wilaya ya Nkasi kuchukua nafasi ya William Mwakalambile ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Nafasi ya Maswi katika PPRA sasa imezibwa na Dennis Simba aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments