WAZIRI MKUU AZINDUA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KIGOMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) aliweka mkono kuashiria uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo Julai 20,2024 Mkoani Kigoma. Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura umeanza rasmi leo katika mikoa ya Kigoma, Katavi na tabora na zoezi hilo linafanyika kwa siku saba hadi tarehe 26 Julai, 2024.
Afisa Mwendesha vifaa (BVR) Bw. Nicholaus Natay akimpiga picha Bi . Josephina Sikabwe mkazi wa Mtaa wa Kawawa Kata ya Kipampa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji mkoani Kigoma kuwa Mpiga Kura. Josephina ndiye mwananvchi wa kwanza kuandikishwa katika daftari la kudumu la Wapiga kura. 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akimkabidhi Kadi ya Mpiga Kura Bi . Josephina Sikabwe mkazi wa Mtaa wa Kawawa Kata ya Kipampa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji mkoani Kigoma baada ya kujiandikisha kuwa Mpiga Kura. 
Bi . Josephina Sikabwe mkazi wa Mtaa wa Kawawa Kata ya Kipampa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji mkoani Kigoma akiwa mwenye furaha baada ya kukabidhiwa Kadi yake. 
*************
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) akigusa kishikwambi kuzindua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura leo tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma. 

Mhe. Majaliwa baada ya kuzindua zoezi hilo alipata fursa ya kushuhudia kuandikishwa kwa mpiga kura na kumkabidhi kadi yake. 

Awali wakati akihutubia wananchi waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika uwanja wa Kawawa uliopo Halmashuauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Mhe. Majaliwa amewataka raia wote wa Tazania wenye sifa wajitokeze kujiandikisha kuwa wapiga kura na kuhakikisha kuwa wasio raia wa Tanzania hawaandikishwi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa iwe kwa kurekebisha taarifa au kuhama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda lingine asisite kufika katika kituo cha kuandikisha kwani Tume imeshajipanga ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa”

 

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa zoezi hilo lina lengo la kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanapata na kutumia haki yao ya kikatiba kama ilivyobainishwa kwenye Ibara ya 5 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

 

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amelitaka Jeshi la Magereza kuweka miundombinu wezeshi ili kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutekeleza wajibu wake wa kuandikisha wafungwa wenye vifungo chini ya miezi sita na mahabusu kwa ufanisi.

 

“Hii fursa ambayo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya kuwawezesha magereza kupiga kura ya kuchagua viongozi wanaowataka, hii mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kutoa fursa kwa wafungwa na mahabusu kupiga kura wakiwa magerezani” 

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewahakikishia watanzania kuwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuhakikisha kuwa chaguzi zote  zitakuwa huru na Haki.


Mhe. Majaliwa  amesisitiza kuwa zoezi hilo ni kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi na kwamba wasio raia wa Tanzanai hawahusiki.

“..anayetakiwa kaundikishwa hapa ni raia wa Tanzania tu. Hapa ni lazima tuwe wazalendo. Tusiruhusu mtu yeyote kutoka nje kujandikisha kuwa mpiga kura,” amesema.

Mhe. Majaliwa pia amevitaka vyama vya siasa kutumia ruhusa ya kisheria ya kuweka mawakala kila kituo, kuhakikisha wanachagua mawakala ambao wanatoka kwenye maeneo vilipo vituo vya kuandikisha wapiga kura ili wawaze kuwatambua watu wanaojiandikisha na uraia wao.

“Mawakala wa vyama vya siasa mnaowajibu wa kuwatambua wanaojiandikisha, naomba nisisitize hapa, lazima muwe wazalendo namba moja, uzalendo wenu utasaidia kuwatambua watu ambao sio raia.”

 

Kwa Upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiandanga amesema kuwa uzinduzi wa uandikishaji na uboreshaji, mchakato huo umeshirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi ikiwa ni utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

“Tume imekutana na wadau wa makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia,Viongozi wa Dini, Makundi Maalum kama vile Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu . Lengo ni kuhakikisha kuwa mchakato huu unakuwa shirikishi kwa watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa au dini”

 

Naye, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele amesema kuwa Jumla ya vituo 40,126 vitatumika katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hivyo, vituo 39,709 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Tanzania Zanzibar. 

 

“Idadi hii ya vituo ni ongezeko la vituo 2,312 zaidi ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika kuandikisha Wapiga Kura kwa mwaka 2019/2020”.

Wananchi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo. 

Viongozi na wazee wa kimila nao ni wadau wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi hivyo nao walihudhuria. 



Viongozi wa vyama vya siasa ni wadau wakuu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, nao waliokuwa ni miongoni mwa walioshiriki katika uzinduzi huo. 

Wasanii Peter Msechu, Sande Linex na Dulla Makabila nao walishiriki kwa kutoa burudani kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma waliohudhuria uzinduzi huo wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura mkoani Kigoma. 









Kundi maarufu la ngoma za asili la Mapigo 7 wakitoa burudani. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments