Katika kuhakikisha mazingira yanaendelea kutunzwa, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii imekuja na mradi wa majaribio ya teknolojia ya Tanuri la kukausha mbao kwa nguvu za jua ambayo ni rafiki kwa mazingira kwa sababu inazuia matumizi ya nishati nyingine ambazo zinaharibu mazingira.
Mkufunzi Msaidizi kutoka Idara ya Uhandisi Misitu na Sayansi za Mazao ya Misitu, Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii Mbonea Mweta amesema mradi huo unafaida utasaidia kuongeza thamani ya mbao na kupunguza gharama kwa wachakataji kwa sababu tanuri hilo linatumia nguvu za jua ukilinganisha na matanuri mengine yanayotumia nishati ya umeme au mafuta ya dizeli ambayo siyo rafiki kwa mazingira.
Tanuri hili kama nilivyosema linasaidia kupata mbao iliyokaushwa vizuri ambayo ina vigezo vya viwango vinavyotakiwa katika mbao na ukitumia mbao iliyokaushwa ni dhahiri kuwa utapata samani nzuri lakini ukiunganisha mbao ambazo hazijakaushwa vizuri ni wazi kuwa utapata changamoto ya muungo huo kuachia au mbao hizo kuharibiwa na wadudu waharibifu na hivyo kupata hasara, amesema Mkufunzi huyo.
Kukamilika kwa mradi huo utasaidia kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuiongezea mapato serikali kupitia biashara ya kukausha mbao hapa nchini kwa kupitia tanuri linalotumia nishati ya jua pekee ambayo ni rafiki kwa mazingira.
Pia mradi huo utakapokamilika na kuanza kutumika wafanyabiashara wa mbao watanufaika kwa kiasi kikubwa, ushauri kwa watengenezaji wa samani kutumia mbao zilizokauka ili kuondoa malalamiko ya wateja wao wanaolalamikia samani zao kuharibiwa na wadudu waharibifu.
0 Comments