Vijana 150 Iringa Kupatiwa Ujuzi Wa Kujiajiri

VIJANA 150 wenye umri wa miaka kati ya 15 na 24 walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu mkoani Iringa, watapata fursa ya mafunzo ya kubadilisha maisha yao kupitia Mradi wa Ujuzi wa Kujiajiri kwa Vijana unaotekelezwa na Shirika la Lyra in Africa.

Mradi huo unaofadhiliwa na Swisscontact, na utakaotekelezwa kwa miezi tisa katika kata ya Isalavano katika halmashauri ya Mafinga Mji na kata ya Kiwele na Nzihi katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, umetambulishwa kwa wadau wake leo.

Mratibu wa mradi huo, Gift Mafue alisema; “Vijana hawa waliohitimu elimu ya msingi na sekondari lakini walishindwa kuendelea na masomo ya juu, sasa wamepewa nafasi ya kujifunza ujuzi muhimu wa maisha na kiuchumi kupitia ajira binafsi.”

Alisema mradi huo una nguzo kuu mbili ikiwemo ya stadi za maisha inayolenga kuwajengea vijana hao uwezo wa kujitambua, kujiamini na kupata mwanga utakaowawezesha kujua fursa mbalimbali za kiuchumi wanazoweza kuzitumia kujiajiri katika vijiji vyao.

“Kwa kupitia nguzo hii, vijana hao watafundishwa pia elimu ya fedha na utamaduni wa kujiwekea akiba ili kukuza mitaji na shughuli zao,” alisema Mafue.

Alisema nguzo ya pili inahusu mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri ambayo itajikita katika maeneo makuu matatu likiwemo la ufugaji wa kuku.

Katika eneo hilo alisema vijana hao watajifunza aina bora za kuku na mbinu za ufugaji bora ili kupata matokeo mazuri kiuchumi.

Akizungumzia eneo la pili alisema vijana hao watafundishwa mbinu za kisasa za kilimo cha mbogamboga, uyoga, mchicha nafaka, na mazingira na nishati mbadala.

“Kuhusu utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati mbadala ya kupikia, vijana wataelimishwa namna ya kutumia sekta hiyo kukuza vipato vyao, ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa vitalu vya miti ya matunda,” alisema.

Alisema mafunzo haya kwa ujumla wake yatawapatia vijana hao ujuzi wa vitendo ambao wanaweza kuutumia moja kwa moja kujiajiri na kubadilisha maisha yao katika mazingira wanayoishi.

Naye Meneja wa miradi wa taasisi hiyo ya Lyra Nora Mkenda alisema vijana watakaochaguliwa ni lazima wawe na uwezo wa kutumia ujuzi watakaopata kwa vitendo na kuhamishia kwenya jamii zao.

Alitoa wito kwa wakufunzi wa vijana hao kusaidia kuchagua vijana wenye moyo na dhamira thabiti, na ambao kazi watakazojifunza zina soko ili kuleta tija kwa haraka.

Akifungua kikao hicho, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Iringa, Sauda Mgeni aliwahimiza vijana watakaochaguliwa kuhakikisha wanatumia mafunzo hayo kwa umakini ili kuleta matokeo sahihi katika kukabiliana na changamoto ya ajira.

“Serikali imeruhusu mradi huu kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya vijana na mafunzo yatakayotolewa ni lazima yawe yale yanahusu mradi huo na si vinginevyo,” alisema na kuongeza kwamba wadau wa mradi wanataka kuona matokeo mazuri na uendelevu.

“Vijana wa Iringa sasa wanayo fursa ya kujifunza ujuzi ambao utawasaidia kuboresha maisha yao na kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yao kupitia mradi huu,” alisema .

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments