BILIONI 11.8 KUENDELEA KUTOKOMEZA MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE


Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hadi kufikia sasa Tanzania imepokea Shilingi Bilioni 11.8 kutoka Serikali ya Uingereza ikiwa ni mchango mkubwa wa kuisaidia Tanzania kukabiliana na magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele ikiwepo Matende, Mabusha, Uono afifu, Usubi na Kichocho tangu mwaka 1998.

Waziri Mhagama amesema hayo leo Septemba 17, 2024 baada ya kikao cha majadiliano na mke wa mtoto wa mfalme kutoka Uingereza Bi.  Sophie Hellen Rhys-Jones jijini Dar Es salaam. 

Amesema, fedha hizo zimesaidia kusomesha wataalam wa Sekta ya Afya, kufanya oparesheni, vifaa tiba pamoja na kutoa kinga tiba katika baadhi ya maeneo yenye wagonjwa wa Trakoma ambao kwa kawaida unaweza kusababisha upofu.

“Mahusiano mazuri ya kidiplomasia ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mataifa mengine yameleta wadau mbalimbali ambao wasaidia sekta zote ikiwemo sekta ya Afya." Amesema Waziri Mhagama na kuongeza

"Tumepata ugeni mkubwa sana nchini kwa kutembelewa na mke wa mtoto wa mfalme kutoka Uingereza na amekuja kuangalia shughuli zetu lengo la ujio wake ikiwa ni kuona na kuhakikisha jinsi Serikali ya Uingereza inavyoweza kusaidia kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele." Amesisitiza Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amefafanua kuwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) linataka hadi kufikia mwaka 2030 tuwe tumekwisha kupambana na magonjwa hayo yote na yameondoka katika nchi zetu, "Tanzania tumejipang hadi mwaka 2027 tuwe tumevuka asilimia 95."

Kuhusua Bima ya Afya kwa wote Mhagama ameiomba Serikali ya Uingereza kushirikiana na Tanzania juu ya mfuko wa bima ya afya kwa wote ili kuwasaidia wananchi wenye hali ya chini kuwa na uwezo wa kupata huduma pindi wanapoitaji bila kupata kikwazo cha fedha. 

Waziri Mhagama ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kudumisha usafi kwa kunawa mikono ,uso, ili kudhibiti magonjwa hayo yasiyopewa kipaumbele

Kwa upande wake meneja mpango wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya Dkt. Clara amesema serikali ya Tanzania chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan imeweza kuwakinga wananchi wengi kutopata ulemavu wa kudumu kutokana na magonjwa hayo yasiyopewa kipaumbele

“Magonjwa haya yana waathiri sana watu wenye kipato cha hali ya chini, serikali imeweka afua mbalimbali kuhakikisha tunatokomeza haya magonjwa ambapo afua hizo ni pamoja na umezeshaji wa dawa za kinga tiba, upasuaji na matibabu kwa walioathirika.” Amesema Dkt Clara








TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments