Mbunge wa Jimbo la Momba Mkoani Songwe Mhe. Condester Michael Sichalwe (Mundi), ameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya ziara ndani ya jimbo lake hilo ili kujionea usumbufu wanaoupata wananchi wa vijiji mbalimbali kutokana na mashamba yao kuchukuliwa na Wakala wa Uhifadhi wa Mistu Tanzania TFS.
Kwa mujibu wa Mbunge Condester baada ya maeneo kadhaa kuchukuliwa na TFS kumesababisha wananchi wake kukosa ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.
Mhe. Condester Sichalwe, amewasilisha ombi hilo Septemba 03, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hii ni kufuatia kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ambao mashamba yao yamechukuliwa na Serikali kupitia wakala huo wa uhifadhi wa misitu Tanzania.
Wananchi wanaokabiliwa na kadhia hiyo ni wale wa vijiji vya, Tontela, Mbalwa, Moravian na Itumbula katika jimbo la Momba mkoani Songwe na wizara ya maliasili na utalii nchini Tanzania imeahidi kufika jimboni Momba kujionea hali halisi baada ya kuahirishwa kwa bunge linaloendelea jijini Dodoma
0 Comments