MJITOKEZE KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA NA MWENDE MKAPIGE KURA - RC

 

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani ametoa onyo kwa wananchi watakaokwenda kinyume na taratiibu za uchaguzi na kufanya making sa ambayo yatawatia hatiani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Nobemba, 27 mwaka huu.

Dkt Buriani ametoa onyo hilo Jana ofisini kwake akizungumza na waandishi wa habari na kuainisha makosa kadhaa yatakayomtia hatiani mwananchi au mjumbe yeyote anayegombea katika uchaguzi huo.

Amesema ni endapo ataharibu orodha ya wapiga kura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi, pili endapo atatoa taarifa za uongo kuhusu Uraia wake, lakini pia kama atajiandikisha zaidi ya mara moja ikiwa ni pamoja na kupiga kura zaidi ya mara moja kwa wagombea wa nafasi moja.

Kosa lingine ni kutishia wapiga kura au wagombea ili kuvuruga uchaguzi, lakini pia kufanya kampeni siku ya uchaguzi, kuonesha ishara au kuvaa mavazi yanayoonesha yanayomtambulisha mgombea au chama cha siasa mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura.

Amesema kosa lingine ni kumzuia msimamizi wa uchaguzi au msimamizi wa kituo atakayeteuliwa kutekeleza majukumu yake, kukiuka masharti ya kiapo chake, kupatikana Kwa karatasi ya kupigia kura zaidi ya moja kwa nafasi moja aliyogombea.

"Makosa yapo kadhaa ikiwamo na mjumbe au mwananchi yeyote atabainika kuvuruga au kuvunja ratiba ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi, kukutwa na silaha kwenye eneo la uteuzi wa wagombea" amesema.

Lakini pia endapo atatangaza matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa rasmi na msimamizi wa uchaguzi lakini pia kufanya jambo lolote kinyume cha kanuni za uchaguzi pamoja na sheria nyingine za nchi zinazohusiana na uchaguzi.

"Makosa haya yanapotokea na mtu yeyote atakayepatikana na hatia za kosa lolote la uchaguzi atahukumiwa adhabu ya faini isiyozidi sh laki tatu au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja,

"Hivyo ni vizuri wananchi wakajua makosa haya ili wasije kujikuta kwenye matatizo bila kujua, wito wangu kwa wakazi wa Mkoa wa Tanga, ninawasihi sana, wote wenye umri wa kuanzia miaka 18 au wale watakaofikisha umri huo siku ya kupiga kura" amesisitiza.

Sambamba na hayo amewataka wananchi kujiandikisha tena kwenye daftari la mpiga kura ifikapo Octoba 11, ili wasipoteze haki ya kuchagua viongozi wanahitajika kwa maendeleo ya Mkoa pamoja na kwenye maeneo yao na pia wasipoteze haki yao ya kikatiba.

Baadhi ya wananchi wameiomba serikali kuboresha huduma kwenye vituo vya kujiandikisha na kupigia kura, ikiwa ni pamoja na muda wa kujiandikisha uongezwe kwakuwa siku 10 pekee hazitatosha kwani wengi wanabanwa na muda wa kutekeleza majukumu yao.

"Tunaona wakati mwengine kunatokea matatizo mbalimbali, suala la huduma ya kwanza ni muhimu sana kwani kwenye maeneo ya kupigia kwakuwa wengine ni wazee lakini pia kuna wagonjwa" amesema Mohamedi Dondo, Karibu wa Wazee Asili, Wilaya ya Tanga.

"Kama wazee, tunawashawishi vijana wetu waweze kujiandikisha na kwenda kupiga kura, lakini pia tunaiomba serikali kuongeza muda wa kujiandikisha katika daftari la mpiga kura, siku walizoweka ni kidogo sana ikilinganishwa na shughuli zetu za kujitafutia kipato" amesema.

Naye Majid Shali amesema, "nikiwa kijana nimejiandaa vizuri na uchaguzi, ni haki ya kila Mtanzania, kumekuwa na tabia ya vijana wengi kukataa kwenda kupiga kura kisha tunalalamikia viongozi hawafai,

"Ili kupata viongozi bora ni lazima tujitokeze na kujua kura ni haki zetu na tunapaswa kujumuika ili kuchagua viongozi bora ambao tutawachagua sisi na siyo kusubiria kuchaguliwa na watu wengine" amefafanua.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments