BRELA KUWAKUTANISHA WADAU KUJADILI FURSA NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI

 

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wameandaa Mkutano wa Pili wa BRELA na Wadau utakaofanyika Oktoba 25, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Oktoba 23, 2024 na Kitengo cha Habari na Mawasiliano BRELA, imesema mkutano huo wa pili kufanyika utawakutanisha wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.


TAARIFA hiyo ilisema lengo la mkutano huo ni kuwaleta pamoja wadau kujadili fursa, mafanikio na changamoto zinazowakabili wadau wake na Sekta ya Biashara kwa ujumla.


Mkutano huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano baina ya BRELA na wadau wake kutoka Sekta ya Umma na Binafsi ikiwa ni pamoja na kuwajengea uelewa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na BRELA na Taasizi zingine zinazoratibu urasimishaji wa biashara nchini.


"Kauli mbiu ya Mkutano huu ni “Mifumo ya Kitaasisi inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara nchini” (Interoperability of Institutional Systems and Business Facilitation)," imeeleza taarifa hiyo na kuongeza,


Taarifa hiyo iliongeza kuwa Kauli mbiu hiyo inakwenda sambamba na maagizo na maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha kuwa mifumo yote inasomana ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu. kwa kuwa urasimishaji wa biashara ni mchakato, ni vema kupitia Mkutano huu Sekta za Umma zinazoratibu urasimishaji wa Biashara nchini wakasikiliza namna bora ya Sekta Binafsi inavyopenda ihudumiwe kupitia mifumo kusomana.


Kutokana na uzoefu uliopatikana katika Mkutano wa kwanza wa wadau wa BRELA uliofanyika Oktoba 27, 2023 na kuhudhuriwa na washiriki wapatao 350 ambao ulitoa mwanga na kuonesha umuhimu wa kukutana na kukaa pamoja na wadau kila mwaka ili kubaini fursa, mafanikio na changamoto wanazokabiliana nazo na kuzipatia ufumbuzi.


Kwani Mikutano kama hii kwa kiasi kikubwa inasaidia kupata uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kupata majawabu ya fursa, mafanikio na changamoto. Inatarajiwa katika Mkutano huu, wadau wataweza kupata mrejesho wa majukumu yanayofanywa na BRELA," imebainisha taarifa hiyo


Hivyo watapata mrejesho wa maoni, ushauri na mapendekezo ya wadau kwenye Mkutano wa BRELA na Wadau wake uliofanyika mwaka jana pamoja na kujadili mada kuhusu mifumo ya Taasisi za Serikali kusoma na uwezeshaji kibishara nchini.


Washiriki wa mkutano huo wataweza fursa ya kupata mrejesho wa huduma za BRELA pamoja na kuweka mkakati ya pamoja ili kuboresha huduma zinazotolewa na kupata maoni juu ya utendaji kazi wa BRELA hasa matumizi ya mifumo kwa kusomana na mifumo ya Taasisi zingine.

Pia, kubaini changamoto zinazowakabili wadau na kuzitafutia ufumbuzi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kukuza uelewa wa wadau kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utoaji wa huduma za usajili na ulinzi na utoaji Leseni ili kuimarisha utekelezaji wa sheria za nchi.

Sambamba na Kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Biashara nchini ikiwemo fursa zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia na namna yanavyochochea ukuaji wa biashara.

Mkutano wa mwaka huu utawakutanisha wadau zaidi ya 300, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za umma, sekta binafsi, Taasisi miamvuli, wafanyabiashara, wanazuoni, wajasiriamali na Mawakili kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Pia mkutano huu utakuwa sehemu ya kubadilishana uzoefu utakaowezesha kuboresha na kuimarisha huduma pamoja na kuongeza ufanisi na tija kwenye utoaji wa huduma na utasaidia kutatua changamoto wanazokutana nazo wateja na wadau wa BRELA utaendeshwa kwa muundo wa Mdahalo ambapo watoa mada, wachagizaji na waongoza mijadala kuhusiana na mada zilizopo wataweza kichangia na kuibua mjadala kulingana na mada husika pamoja na kauli mbiu ya Mkutano huu wa pili.

Mkutano wa mwaka huu ambao utawakutanisha washiriki wapatao 300 umepewa kauli mbiu “Tunaipa uhai wa kisheria biashara yako” itatumika katika kuakisi mada zitakazo tolewa kwa kuzingatia ushiriki wa wadau waliopo kwenye mnyororo mzima wa urasimishaji na ufanyaji wa biashara nchini

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments