Ikiwa imebaki siku moja kuelekea uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Orodha ya Wapiga kura(Daftari la Makazi),Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe,Nurdin Babu amewahasa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutoka majumbani kwao na kwenda kujiandikisha katika Daftari la Orodha ya Wapiga kura ili kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27.
Mhe.Babu ameyasema hayo leo tarehe 10 Oktoba,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari,ambapo amesema kuwa zoezi la kujiandikisha katika Daftari hilo litaanza kesho tarehe 11 Oktoba,2024 hadi tarehe 20 Oktoba,2024 katika vituo vya kujiandikishia vipatavyo 2,368 Mkoa mzima.
Aidha Mhe.Babu ameeleza kuwa Nchi ya Tanzania,ni Nchi huru na ya demokrasia ambapo wananchi wanapaswa kuamua kuhusiana na namna ya kuendesha masuala ya msingi kuhusiana na serikali zao hususani Serikali za Mitaa.
Sambamba na hilo RC Babu amezitaja sifa za wanaojiandikisha kwenye Daftari la Orodha ya Wapiga kura kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,ambazo ni lazima awe raia wa Tanzania,awe na umri wa miaka 18 au zaidi,awe mkazi wa Kijiji au Kitongoji au Mtaa ambao Uchaguzi unafanyika,awe na akili timamu na awe amejiandikisha kupiga kura katika Kitongoji,Mtaa au Kijiji husika.
Vituo vya kujiandikishia vitafunguliwa kuanzia saa mbili kamili (2:00) asubui na kufungwa saa 12:00 jioni na uandikishaji utafanyika ndani ya siku 10, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 umebeba kauli mbiu isemayo "Serikali za Mitaa Sauti ya Wananchi Jitokeze Kushiriki Uchaguzi.
0 Comments