Dar kuanza na maeneo saba biashara saa 24.

DAR ES SALAAM; MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Jiji la Dar es Salaam litakapoanza kufanya biashara saa 24 mapato yataongezeka na uchumi utakuwa kutokana na kuongezeka kwa wigo wa biashara.

Chalamila alisema hayo alipomtembelea Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda ofisini kwake Dar es Salaam jana.

Alisema uzinduzi wa biashara saa 24 unatarajiwa kufanyika Februari 27, mwaka huu.

Chalamila alitaja maeneo yatakayoanza kufanya biashara saa 24 kuwa ni Kariakoo, Magufuli Terminal, Tandika, Mbagala, Bunju, Manzese na Mwenge.

“Tunatarajia kuongeza idadi ya wafanyabiashara kupitia kufanya biashara saa 24 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo litaongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi kwa upande wa TRA,” alisema.

Chalamila alisema biashara zote zitasajiliwa na kupatiwa leseni kwa upande wa halmashauri na namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa upande wa TRA kurahisisha ulipaji kodi.

“Tayari tumeanza kukaa na kuzungumza na wadau mbalimbali wakiwemo wa usafirishaji ili na wao waanze,” alisema.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alisema TRA ipo tayari kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha biashara inafanyika saa 24.

Mwenda alisema watahakikisha kunakuwa na ustawi wa biashara pamoja na utulivu jambo ambalo litawavutia watu wengi zaidi kuingia kwenye biashara saa 24.

Alisema miongoni mwa majukumu ya TRA ni kusimamia ustawi wa biashara, hivyo mahala popote panapogusa kuweka mazingira mazuri ya biashara TRA ipo tayari kusaidia ili kuweka mazingira rafiki na mazuri kwa walipakodi kufanya biashara zao.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments