Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, ameweka wazi kuwa timu yake haitaki kujiwekea presha kwa kufikiria zaidi mchezo wa ‘Kariakoo Derby’, badala yake inajikita kikamilifu katika mechi yake Februari 28 ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji.
Yanga itakuwa ugenini dhidi ya Pamba katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kamwe amesema licha ya mashabiki na wadau wa soka kuzungumzia ‘Kariakoo Derby’, wao wanazingatia zaidi mchezo wao wa ligi dhidi ya Pamba.
“Hatutaki kujitia presha kwa kuwaza Kariakoo Derby. Hatutachukua ubingwa kwa kushinda mechi moja pekee, tunapaswa kushinda kila mchezo kabla ya kumkabili mpinzani wetu, Simba, Machi 8.
“Tumejifunza kutokana na makosa ya nyuma. Tukumbuke kuwa Simba walitoka sare dhidi ya Fountain Gate FC kule Manyara, na baadaye sisi tukatoka sare na JKT Tanzania. Hili linapaswa kuwa funzo kwetu. Simba wametoka sare na Azam FC, lakini hatupaswi kuwachukulia kwamba wametoka kwenye mbio za ubingwa. Bado tuna mechi ngumu mbele yetu,” amesema Kamwe.
Pia amesisitiza kuwa wanapaswa kuzingatia mchezo huo dhidi ya Pamba Jiji badala ya kufuatilia sare ya Simba na Azam FC.
“Tunahitaji kushinda huu mchezo na kupata alama tatu. Sio lazima tucheze soka la kuvutia au tufunge mabao mengi huku tukiruhusu mabao mengi pia. Mwisho wa siku kinachoangaliwa ni alama tatu, siyo urembo wa mpira,” amneongeza Kamwe.
0 Comments