SERIKALI inaendelea kutekekeza miradi kwa lengo kupunguza misongamano ya magari katika majiji na miji mikubwa.
Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu katika Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Ephatar Mlavi amesema hayo wakati akitoa taarifa kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo kujiandaa kuadhimisha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Mlavi amesema hayo Dodoma kuwa baada ya shughuli za serikali kuhamia Dodoma, kumekuwa na ongezeko la magari.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa serikali imeweka juhudi kuhakikisha Dodoma haiathiriwi na msongamano wa magari.
Alitaja baadhi ya jitihada hizo ni ujenzi wa barabara ya mzunguko ya njia nne yenye urefu wa kilometa 112.3 ambao unatekelezwa katika vipande viwili.
Mlavi alisema kipande cha kwanza kutoka Nala kwenda Veyula, Mtumba hadi Bandari Kavu Ihumwa chenye urefu wa kilometa 52.3, ujenzi umefikia asilimia 91 huku kupande cha pili chenye kilometa 60 kutoka Bandari Kavu Ihumwa kwenda Matumbulu hadi Nala ujenzi wake umefikia asilimia 84.
Alisema pia serikali inatekeleza mradi wa upanuzi wa barabara kuu nne zinazoingia mkoani Dodoma kutoka mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Iringa na Singida.
“Serikali imepanga kupanua kilometa 70 njia ya kuingilia kutoka Dar es Salaam, kilometa 50 njia kutokea Arusha, kilometa 50 njia ya kutokea Singida na kilometa 50 kwa njia ya kuingilia kutoka Iringa na kufanya jumla ya kilomita 230,” alisema Mlavi.
Alisema serikali imepata fedha kutoka Benki ya Dunia kutekeleza mradi huo na kubainisha kuwa ipo katika hatua za awali kuanza kutekeleza kwa awamu ya kwanza.
Mlavi alisema awamu ya kwanza itahusisha kilometa 40, na kilometa 32 zitapanuliwa kutokea Dodoma hadi Chamwino ambayo itapanuliwa kwa njia nne na njia sita katika baadhi ya maeneo na kubainisha kuwa mradi huo upo katika hatua za manunuzi.
“Barabara zingine za awamu hii ya kwanza ni barabara ya kutokea eneo la Bahi kwenda Msalato kilometa 10.7 itajengwa kwa njia nne na kipande kingine ni kutoka mzunguko wa Image kwenda Mkonze kilometa saba na yenyewe itajengwa kwa njia nne,” alifafanua Mlavi.
Aidha, alisema katika vipande hivyo viwili serikali ipo katika hatua za mwisho kuandaa nyaraka ili kutangaza zabuni ili apatikane ambaye atajenga barabara hizo.
Alisema katika Jiji la Mbeya miradi inayoendelea ni pamoja na upanuzi wa barabara ya Msagala – Ifisi wa kilometa 29 unaohusisha njia nne umefikia asilimia 19.3.
Alitaja mradi mwingine ni barabara ya Igawa, Sungwi na Tunduma kwamba upanuzi wa kilometa 218 unafanyika na serikali imepata mkandarasi ajenge njia nne kupunguza msongamano.
Alisema katika Jiji la Mwanza, kuna mradi wa upanuzi wa barabara ya kilometa 25 kutoka Usagara hadi Mwanza kwa upanuzi wa njia nne.
Alisema mradi huo upo katika hatua ya ununuzi ili kumpata mkandarasi. Kwa Jiji la Arusha, alisema kipande cha kutoka Arusha kwenda Tengeru kimepanuliwa kwa njia nne lakini kipande cha Tengeru kwenda USA hadi KIA na chenyewe kimepangwa kutekelezwa kwa kupanuliwa kwa njia nne.
“Serikali imeshapata fedha kwa kujenga awamu ya kwanza ya kipande hiki cha Tengeru – USA – KIA kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JAICA) kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 11.3 kutokea Tengeru hadi Usa River,” alisema Mlavi.
Alisema katika Mji wa Moshi kupitia mpango wa ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Japan kitajengwa kipande cha kilometa 11.3 kutoka Mailisita kwenda Kibaoni ikihusisha kujenga upya Daraja la Kikavu kutatua changamoto za msongamano na kuimarisha usalama barabarani.
Mlavi alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam tayari mradi wa upanuzi wa barabara ulikamilika ambao ni barabara ya njia nane ya Kibaha – Kimara.
0 Comments