“Msaada wa kisheria muhimu kwa wanyonge- Maswi

MBEYA: WATAALAM wa Utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria inayojulikana kama” Mama Samia Legal Aid (MSLAC) mkoani Mbeya wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuwasaidia  Wananchi kutatua migogoro yao  na kupata haki zao kwa wakati.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi ametoa wito huo wakati akifungua  mafunzo kwa Wataalam hao yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu Kampeni hiyo inayotarajia kuanza  Februari 24 hadi Machi 5 mkoani hapa.

Maswi aliwataka wataalamu hao watakapokwenda kwenye wilaya zao kutekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na  kuacha ubinafsi na upendeleo wakati wa utoaji haki na badala yake waimarishe upatikanaji wa haki kwa usawa ili kufikia malengo ya kampeni hiyo.

“Ukipewa nafasi onesha uwezo wako,nyie Serikali imewaamini na mmepata na mafunzo haya leo ,sasa mkifika kwenye wilaya zenu msisumbue wananchi wasaidieni kwani katika utekelezajiwa Kampeni mtaona malalamiko ya Wananchi yatakavyokuwa mengi,”alisema.

Aliongeza kuwa yapo malalamiko na migogoro ya wananchi ambayo ni midogo na wataalamu hao wana uwezo wa  kutatua na kuwasaidia wananchi wa maeneo yao endapo  wataacha ubinafsi na kutanguliza haki na usawa kwa watu wanaowahudumia.

Awali akieleza kuhusu malengo ya mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Wizara ya Katiba na Sheria,Ester Msambazi alisema kampeni hiyo inatekelezwa na wataalamu wa sheria kutoka kwenye halmashauri hivyo wanawajengewa uwezo wa namna ya kutatua migogoro.

Naye Kiongozi wa  Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Baraka Mbwilo amesema kuwa Wizara imeendelea kushirikiana na Chama hicho katika kuhakikisha kuwa Malengo ya Kampeni hiyo yanafikiwa na Wananchi wenye uhitaji wa Haki wanafikiwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments