Serikali: Tumejipanga Uchaguzi Mkuu

 

DAR ES SALAAM; SERIKALI imesema imejipanga kushirikiana vema na vyombo vya habari kufanikisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu ili uliache taifa likiwa salama.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema hayo Dar es Salaam jana akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari.

Alidokeza kuwa lengo la kukutana na wahariri ni kutengeneza mkakati wa kufanya kazi pamoja kuelekea uchaguzi mkuu utakaotengeneza Tanzania bora kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Alisema vyombo vya habari vina dhima katika uchaguzi kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu na wananchi wanashiriki kwa kutumia haki yao kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa kuliongoza taifa.

Aliongeza kuwa uchaguzi huo lazima uwaache Watanzania wakiwa pamoja kwani kama kukitokea tatizo lawama zitaenda kwa waandishi wa habari hivyo akawasihi wanahabari kutekeleza wajibu wao kwa kuyaweka mbele maslahi ya nchi.

“Sisi sote ni Watanzania na nyumbani kwetu ni Tanzania tuna dhima ya kufanya kazi kuijenga nchi kuwa moja kuelekea uchaguzi na kuiacha ikiwa moja baada ya uchaguzi,” alisema Msigwa.

Aidha, Msigwa alifikisha ujumbe kwa wahariri kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa yuko tayari kuwasikiliza wanahabari na kuwapatia wanachotaka ili kufanikisha majukumu yao.

Alisema serikali haina mpango wowote wa kufungia chombo cha habari na badala yake imefungulia vyombo vyote vilivyokuwa vimefungiwa kutokana na makosa mbalimbali ya kiuandishi.

Msigwa alifafanua kuwa badala ya kufungia chombo cha habari, serikali itawakumbusha wanahabari wanaokengeuka ili kupunguza na kumaliza kabisa makosa yanayoweza kuleta taharuki katika nchi.

Alieleza kupitia Bodi ya Ithibati ambayo itazinduliwa Machi 03, 2025, serikali imejipanga kutoa mafunzo kwa waandishi wa Habari kuhusu namna ya kuripoti uchaguzi mkuu na kwamba mkutano wa kwanza wa Baraza Huru la Habari unatarajiwa kufanyika Aprili, 2025.

“Tunataka katika suala la uhuru wa habari, mifano ya utendaji wa vyombo vya habari katika mazingira huru iwe Tanzania kwa sababu uandishi bora si kuibomoa nchi yako, bali ni kuijenga nchi yako,” aliongeza Msigwa.

Msigwa aliwataka viongozi wa serikali na wa mashirika ya umma kuhakikisha wanashirikiana na waandishi wa habari kwa kuwapatia majibu ya maswali yao kwa sababu katika vitu vinavyowakatisha waandishi tamaa katika kazi yao ni kuwanyima ushirikiano katika majukumu yao.

Kwa upande wa madeni ya vyombo vya habari, Msigwa alisema serikali imepata changamoto kwa sababu vielelezo vinavyoletwa na vyombo vya habari havina nyaraka za kuyathibitisha madeni yao hivyo serikali inaendelea kuvisaidia vyombo vya habari kupata haki zao.

Katika hatua nyingine, Msigwa alisema serikali inaendelea na mchakato wa kufanikisha vitambulisho vya wanahabari vya kidijiti ambavyo vitamtambua mwanahabari popote duniani.

“Tunataka kutengeneza vitambulisho vya waandishi wa habari vya kidijiti na mashine imeshanunuliwa na mfumo unaanza kufanya kazi kwa kutoa vitambulisho vya elektroniki ili waandishi wa mikoani wasiwe na haja ya kuvifuata kuja Dar es Salaam,” alieleza Msigwa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema anatamani uchaguzi mkuu wa mwaka huu uwe uchaguzi wa ajenda, na ajenda hizo zipelekwe katika vyombo vya habari ili ziwe na tija kwa Watanzania.

Balile amehimiza vyombo vya habari vijiandae kuchambua ilani za uchaguzi za vyama na kuwauliza maswali wanaogombea.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments