Tanzania yaimarika tiba za kibingwa za moyo

MABORESHO ya sekta ya afya nchini yanayoendelea kufanywa yameleta mageuzi katika matibabu yakiwemo magonjwa ya moyo.

Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi 2024, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilihudumia wagonjwa 237,132 ikilinganishwa na wagonjwa 93,017 waliohudumiwa kipindi kama hicho mwaka 2022/2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema menejimenti ya taasisi inaendelea kuboresha huduma za tiba ya moyo nchini kwa kufungua matawi ya kutolea huduma hizo na lengo ni kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaotibiwa makao makuu ya taasisi.

“Uhitaji wa huduma za matibabu ni kubwa, kliniki za JKCI tunaziongeza, tumefungua Oysterbay na Kawe Dar es Salaam lakini pia Hospitali ya Dar Group, sasa ya JKCI tumedhamiria kupunguza msongamano wa wagonjwa,” alisema Dk Kisenge.

Alisema JKCI imeendelea kutambulika ndani na nje ya nchi hivyo kuzifanya nchi za Afrika kushirikiana nayo katika kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na nyingine kushirikiana na JKCI katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo.

“Taasisi yetu mwaka 2024 imeweza kufanya kambi ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo nchini Comoro ambapo wagonjwa zaidi ya 2,000 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo na kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo nchini Zambia,” alisema Dk Kisenge.

Aliishukuru serikali kwa kuiwezesha taasisi hiyo kufanya matibabu ya kihistoria barani Afrika.

“Serikali ya Awamu ya Sita imetuwekea vifaa vingi ambavyo vimewezesha wagonjwa wengi na walikuwa hawajui waende kutibiwa wapi kufanyiwa matibabu, hata wenzetu walifurahia aina ya vifaa tulivyonavyo kwa namna vimewawezesha wataalamu wetu kufanya upasuaji wenyewe kwa asilimia 90,” alisema Dk Kisenge.

Alisema JKCI itaendelea kuwa kituo cha utalii tiba ambapo wagonjwa kutoka nchi 20 za Afrika zinafika kwenye taasisi hiyo kupata matibabu.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imebainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano 2020-2025, CCM itaendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania na ustawi wa taifa.

Mei 2024, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025 aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu alisema serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya kwa kuziwezesha hospitali ikiwemo JKCI ili kutoa matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini.

Ummy alisema katika kutekeleza dhana ya ubunifu, JKCI ilianzisha huduma mpya mbili, ya kwanza ni ya ubingwa bobezi ambayo ni kubadilisha valvu ya moyo bila kupasua kifua ambapo matibabu hayo hufanyika nchi chache Afrika na hata hospitali chache katika nchi zilizoendelea.

Alisema kutokana na kuboreshwa kwa huduma za tiba ya moyo nchini JKCI imeokoa Sh bilioni 63 zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya matibabu ya moyo nje ya nchi.

Ummy alisema gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa nchini ni Sh milioni 80.4 na kutibiwa nje ni Sh milioni 220.

Alisema huduma ya kufungua mishipa ya miguuni iliyoziba kwa kuweka kifaa kwenye mishipa mikubwa ya damu iliyopasuka gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa nchini ni Sh milioni sita na kutibiwa nje ni Sh milioni 13.

Aidha, huduma nyingine 136 za ubingwa na ubingwa bobezi zimetolewa katika kipindi cha 2023/2024 ambazo ni pamoja na uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo kwa wagonjwa 120, kufunga vifaa visaidizi vya moyo kwa wagonjwa 93, kuzibua mishipa ya damu ya moyo kwa wagonjwa 105 na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo kwa wagonjwa 87.

Ummy alisema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, JKCI iliendelea kutoa huduma bobezi za upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua na mishipa ya damu kwa wagonjwa 457 ikilinganishwa na wagonjwa 409 waliofanyiwa huduma kama hiyo mwaka 2022/2023.

Kwa matibabu hayo imefanya idadi ya wagonjwa waliofanyiwa huduma hiyo kufika 7,794 tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo mwaka 2015.

Aidha, maboresho mengine yaliyofanywa katika sekta ya afya ni kuwepo kwa huduma ya upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua na mishipa ya damu ambapo gharama zake wastani ni Sh milioni 15.45 kwa mgonjwa mmoja.

Gharama hizo ni nafuu kwani mgonjwa kutibiwa nje kwa huduma hiyo anapaswa awe na Sh milioni 50.8.

Kuhusu hatua zilipopigwa za matibabu ya kisasa katika taasisi ya JKCI, kwa mwaka 2023/2024 jumla ya wagonjwa 1,920 wamepata tiba ya upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu ukilinganisha na wagonjwa 1,790 waliofanyiwa huduma kama hiyo 2022/2023.

Hivyo kwa ongezeko hilo kunafanya idadi ya wagonjwa waliofanyiwa huduma hiyo kufika 33,390 Machi 2024, tangu huduma hizo zianze katika taasisi hiyo ya JKCI.

Kuhusu gharama, imetajwa kuwa upasuaji huo katika taasisi ya JKCI ni wastani wa Sh milioni sita kwa mgonjwa mmoja ikilinganishwa na wastani wa Sh milioni 20 kwa mmoja akitibiwa nje ya nchi.

Kuhusu huduma za kliniki kwa watu mashuhuri, taarifa hiyo inaonesha jumla ya wagonjwa 2,970 walipata huduma hiyo kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024.

Pia, upatikanaji wa dawa kwa magonjwa ya moyo ni asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 90 kipindi kama hiko mwaka 2022/2023.

Mwaka jana mjini Zanzibar wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema zaidi ya wagonjwa 800 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na wengine zaidi ya 2,000 wamefanyiwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo maalumu katika taasisi ya JKCI katika kipindi cha miaka miwili.

Mbali na matibabu hayo kwa Watanzania pia wagonjwa kutoka nchi jirani nao wamepatiwa matibabu na kwa kipindi cha miaka miwili zaidi ya wagonjwa 2,400 kutoka nchi za Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda pamoja na Zambia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments