UWANJA WA MPIRA WA MIGUU WA KIMATAIFA, RASMI KUJENGWA NZUGUNI, DODOMA

                               

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Palamagamba Kabudi, leo Februari ameshuhudia hafla ya utiaji saini Mkataba wa kuanza rasmi Ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu utakaokia na uwezo wa kubeba watazamaji 32,000 waliokaa kwa mara moja katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.

Akizungumza na hadhara iliyojitokeza kushuhudia hafla hiyo, Waziri Prof. Kabudi ametoa wito kwa Mamlaka zinazohusika na vibali vya Ujenzi, kuharakisha upatikanaji wa vibali hivyo ili zoezi lianze mara moja na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

"Ili kukamilisha azma hii kwa wakati, baadhi ya masuala ya muhimu kama kupatikana kwa vibali vya Ujenzi kutoka Ardhi, zimamoto, mazingira, huduma za umeme, maji na Barabara za Mawasiliano zinatakiwa kufika kwenye eneo la Mradi ili kufikia lengo la kuwapa wananchi uwanja wenye hadhi ya Makao Makuu ya nchi". Prof. Kabudi 

Aidha, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Khamis Mwinjuma (MB) amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Mhe. Dkt. Samia, wameweza kufanya mambo mengi kwenye Ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa, uwanja wa Uhuru, uwanja wa kisasa wa michezo Arusha na mingine mingi.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema uwanja huo utagharimu fedha kiasi cha shilingi Milioni 310 ambayo itagharamiwa na Serikali kwa 100% huku Ujenzi wake ukitekelezwa na Kampuni ya Ujenzi kutoka nchini Italia ya Limonta.

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amebainisha kua; "Moja ya vipaumbele vya Mkoa ni utalii wa michezo ikiwemo mpira wa miguu hivyo, tulikua tunaandika uwanja ambao hatujauona kwa macho lakini tukawa tunaishi kwa imani kua uwanja huu utatokea na utaleta watu wengi hivyo, tujipange kwa utalii huu wa michezo uwe na tija kwa wananchi wa Dodoma"

Nae, Mbunge wa Jimbo la Dodoma na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, amempongeza Mhe. Rais kwani wananchi wake walikua na shauku kubwa ya kuona uwanja huo unajengwa hapa Dodoma na leo wameshuhudia tukio kubwa la kihistoria la utiaji saini Mkataba wa kuanza rasmi Ujenzi wa uwanja huo.
Matukio ya picha katika tukio hilo













Na: Hellen M. Minja,
Habari - DODOMA RS 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments