GEITA: JESHI la Polisi mkoani Geita linawashikilia wanafunzi 30 wa kidato cha sita, shule ya sekondari Geita (GESECO) iliyopo mjini Geita kwa tuhuma za kufanya vurugu na kupelekea uharibifu wa mali shuleni hapo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adamu Maro amethibitisha jana taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari na kueleza vurugu hizo zilitokea usiku wa Februari 20, 2025 majira ya saa mbili usiku.
Amesema vurugu hizo zilikuja kufuatia tukio la mwanafunzi mwenzao wa kidato cha sita Brighton Philipo wa mchepuo wa EGM kukamatwa na walinzi akimiliki simu ya mkononi kinyume na taratibu za shule.
“Walinzi walipoichukua ile shule ili waiwasilishe kwa uongozi wa shule, mwanafunzi yule pamoja na wenzake waliweza kufanya vurugu na kuwapiga mawe walinzi.
“Lakini hata hivyo zilitumika nguvu za kadri za walinzi kuwadhibiti na hatimaye wakawanyanganya ile simu na kuiwasilisha kwa uongozi wa shule ambapo mwanafunzi huyo alipewa ‘sunspesion’.
“Lakini wanafunzi wenzake walipokuja kubaini kwamba mwezao amesimamishwa shule basi ndio hapo wakaanzisha vurugu na kuanza kudai kwamba mwenzao arudishwe shule kwamba ameonewa”, amesema.
Amesema wakati vurugu zikiendelea mwalimu wa zamu alitoa taarifa kwa jeshi la polisi ili kudhibiti uharibifu wa mali na hata jeshi la polisi walipofika shuleni hapo wanafunzi walijihami kwa mawe.
“Mwalimu wa zamu aitwaye Lucas Ngurabuto baada ya kupata taarifa ya viashiria vya vurugu alifika na kuwasihi wanafunzi wasianzishe vurugu lakini hawakumsikiliza na wakaishia kumrushia mawe.
“Mwalimu alipata majeraha kidogo na ameshatibiwa na sasa hivi anaendelea na kazi, madirisha ya vioo vya aluminiamu yaliyoharibiwa ni saba thamani yake ni milioni mbili na laki tisa”, amesema Kamanda Maro.
Amesema mbali na uharibifu uliotokea jeshi la polisi lilifanikiwa kutumia nguvu ya kadri kudhibiti uharibifu zaidi huku mwanafunzi aliyekamatwa na simu amesimamishwa masomo mpaka Mei 05, 2025.
0 Comments