Yametimia Bwawa la Nyerere

PWANI; SERIKALI imesema utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) umefikia asilimia 99.8.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika eneo la mradi huo wilayani Rufiji.

Msigwa alisema mambo yaliyobaki kukamilika kwa mradi ni madogo likiwemo la kumalizia mtambo wa tisa ambao umefikia asilimia 98.

“Majaribio yake yanaanza Februari 25, na Machi 10, mtambo huu na wenyewe utaingizwa kwenye gridi ya taifa ya umeme ili tukamilishe megawati 2,115,” alisema.

Aliongeza: “Kuna mahandaki ya kupitisha maji ambayo tumekamilisha kwa asilimia 100 tumejenga jengo la mitambo ambalo ndani yake kuna mitambo tisa na kila mtambo mmoja unazalisha megawati 235, yote tisa yanazalisha megawati 2,115 na hilo limekamilika kwa asilimia 99.96”.

Msigwa alisema sehemu muhimu katika mradi huo ni utekelezaji wa mradi wa kusafirisha umeme kutoka kwenye bwawa hilo hadi Chalinze ambako kunajengwa kituo cha kupooza umeme ili baadaye uingizwe kwenye gridi ya taifa na kwamba hadi sasa kimefikia asilimia 92 na gharama yake ni Sh bilioni 558.

Pia, alisema asilimia 95.9 ya malipo ya wakandarasi wanaofanya kazi kwenye mradi huo yameshafanyika.

“Tumeshalipa Sh bilioni 6.28, tumebakiza kiasi kidogo kama Sh milioni 200 hivi kumaliza kabisa asilimia 100,” alisema.

Msigwa alisema serikali imejipanga kulinda miradi yote ya umeme kwa kuweka askari na kufunga kamera kulinda miundombinu, hivyo yeyote atakayejaribu kuhujumu miundombinu hiyo atajulikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aliwataka wananchi waache kusogelea miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa nia ya kuiba au kutaka kuitumia kama vyuma chakavu, kuepuka hatari ya kunasa na hata kupoteza maisha.

“Msiguse nyaya za umeme, waya wa umeme ukianguka nenda katoe taarifa kwa Tanesco, wataalamu watakuja wataondoa huo waya wataacha eneo likiwa salama lakini usiende na kipanga chako cha kukatia mchicha ukakata waya ili uuze chuma chakavu utanasa,” alionya.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments