Hongera Samia kumuenzi Magufuli


LEO imetimia miaka minne tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kilichotokea katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.

Ni kumbukumbu ya machozi kwa Watanzania kwa kumpoteza rais aliyekuwa madarakani na aliyefanya mambo mengi makubwa, yenye maendeleo kwa ajili ya taifa.

Anakumbukwa kwa msimamo wake wa kupambana na ufisadi, kuboresha miundombinu na kuhimiza uzalishaji wa ndani.

Aliendeleza vyema kazi za watangulizi wake katika sekta mbalimbali na kujielekeza kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi zinanufaisha Watanzania wote.

Magufuli anakumbukwa alivyotekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara na madaraja, pamoja na uimarishaji wa huduma za afya na elimu. Hakika Tanzania itaendelea kumkumbuka Magufuli.

Wakati tukiendelea kuungana na serikali, watu binafsi na wadau mbalimbali kumkumbuka leo Magufuli kwa mema aliyoifanyia nchi, vilevile tunatambua na kumpongeza Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza gurudumu bila kutetereka.

Rais Samia ambaye aliapishwa kuongoza nchi Machi 19, 2021, ikiwa ni siku mbili baada ya kifo cha Magufuli, pia ni sehemu ya maendeleo wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano kwani ndiye alikuwa Makamu wa Rais.

Tunampongeza kwa juhudi za kuendeleza maendeleo ya mtangulizi wake kiasi cha kuleta faraja na matumaini makubwa kwa Watanzania.

Isitoshe, Rais Samia amekuja na mambo mengine mapya na makubwa yanayoimarisha ustawi wa nchi na kila Mtanzania.

Rais Samia ameonesha umahiri katika kuleta mafanikio katika sekta za afya, elimu na uchumi kwa ujumla.

Uongozi wa Rais Samia umejikita pia katika kujenga umoja na mshikamano kati ya wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa rasilimali za taifa.

Ameongoza bila kutetereka huku akiimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mengine, huku akichangia katika juhudi za kuleta amani na utulivu katika Kanda ya Afrika Mashariki.

Amejenga mazingira bora ya biashara, amevutia wawekezaji wengi jambo ambalo linatia nguvu uchumi wa Tanzania.

Ni wazi kwamba Watanzania tunamkumbuka Magufuli chini ya falsafa yake ya ‘Hapa Kazi tu’ ambayo iliidhihirisha; lakini tukiwa na faraja na matumaini makubwa kutokana na uendelevu wa uchapa kazi chini ya Rais Samia.

Hakika Rais Samia chini ya falsafa yake ya ‘Kazi Iendelee’ ameitendea haki safari ya maendeleo ya Tanzania aliyoianzisha Magufuli wakati wa awamu ya tano.

Tunamtakia kila heri Samia na kuitakia nchi yetu ufanisi na mustakabali bora zaidi wa amani, upendo na utulivu kama ambavyo serikali yake imejizatiti kuyaendeleza.

Aidha, tunakumbusha umma wa Watanzania na viongozi kwa ujumla, kuzingatia utamaduni wa kurithi fikra na maono mema ya watangulizi kwa mustakabali mwema wa kizazi kijacho tukihimiza ‘Kazi Iendelee’.  Hongera Rais Samia kwa kuenzi mema yote ya Serikali ya Awamu ya Tano.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments