KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeshauri serikali kuongeza usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Tatu kutoka katikati ya mji Posta hadi Gongo la Mboto, Dar es Salaam, ili ikamilike kwa wakati kama ambavyo mkataba unavyoonesha na hivyo kuondoa changamoto ya msongamano.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Seleman Kakoso, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara ya kukagua Ujenzi huo ambao umefikia asilimia 81 ambapo amesema pamoja na kuridhishwa na Ujenzi huo lakini Wana wasiwasi unaweza usikamilike kwa wakati.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi upo wa mradi upo nyuma kwa asilimia moja na kwamba kilichokwamisha ni uondoaji wa baadhi ya miundombinu mingine ikiwemo ya maji na umeme katika barabara hiyo huku akiahidi kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu utakuwa umekamilika.
Naye Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Frank Mbilinyi amesema ili kukamilisha kwa wakati ujenzi huo amewaomba watumiaji wa vyombo mbalimbali vya usafiri kuacha kuingia maeneo ya ujenzi pamoja na wananchi kuacha kufanya biashara sehemu za ujenzi kwa kuwa wanahatarisha usalama wao.
Kamati hiyo pia imeitembelea Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA) na kuagiza serikali kuwalipa fidia wananchi wanaotakiwa kuhamishwa, ili kupisha sehemu ya kupaki magari upande wa Kigamboni, Dar es Salaam pamoja na kuharakisha matengenezo ya Kivuko cha MV Magogoni, ambacho kinafanyiwa matengenezo Mombasa, Kenya, ili kutoa huduma kwa wananchi.
0 Comments