Majaliwa: Toeni mafunzo yanayozingatia soko la ajira

Waziri Mmku Kassim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini kutoa mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.
Ametoa wito huo leo Machi 18 katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Mahitaji ya soko la ajira tutayajua kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema katika zama hizi zenye kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa VETA kuendelea kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.
“Toeni mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia, mafunzo hayo yajumuishe ujuzi wa teknolojia za kisasa zinazochochea uzalishaji wenye tija,” amesisitiza Majaliwa.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa Elimu ya Ufundi Stadi, Majaliwa amesema takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonesha takribani asilimia 70 ya ajira zote ni ajira binafsi na kwa watu wenye elimu ya ufundi stadi hasa kwenye sekta za kilimo, ujenzi, usafirishaji, na huduma za kijamii.
“Kwa upande wa nchi yetu, takwimu za ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2020 na 2024 zinafikia Milioni 7 ambapo ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi imeajiri watu milioni 6.1 sawa na asilimia 87.1 . Wengi wao wana elimu ya ufundi stadi, na sekta rasmi imeajiri watu 907,873 (asilimia 12.9) ambapo wengi wao ni wale wenye elimu ya juu,” amesema.
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi unakamilika haraka.
Majaliwa amesema ukamilishwaji wa vyuo hivyo vinavyojengwa na Serikali unalenga kutimiza dhamira ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania kiujuzi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments