TLS yawajengea uwezo mabaraza ya ardhi ya kata Iringa.

 

KUTOKANA na changamoto ya baadhi ya mabaraza ya ardhi ya kata kutoa maamuzi badala ya kusuluhisha, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa kimefanya mafunzo elekezi kwa wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata za Manispaa ya Iringa.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wajumbe kuhusu wajibu wao wa kisheria na umuhimu wa kusimamia usuluhishi kwa haki na kwa kuzingatia taratibu za kisheria.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, amewataka wajumbe wa mabaraza kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa haki, uadilifu na kwa kuzingatia sheria.

“Hela za hongo haziwezi kukufikisha popote. Tendeni haki na msipoona suluhisho, pelekeni suala husika katika ngazi za juu kwa msaada zaidi,” alisema Kheri James huku akiipongeza TLS kwa juhudi zao za kutoa elimu ya sheria na kusaidia kutatua migogoro ya ardhi.

Aidha, aliwakumbusha wajumbe wa mabaraza kuwa wao ni madaraja kati ya wananchi na vyombo vya juu vya utatuzi wa migogoro, hivyo wanapaswa kuwa wasikivu, wavumilivu na kutumia maarifa ya sheria pamoja na mila za jamii husika ili kufanikisha maridhiano.

Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Iringa, Moses Ambindwile amesema mabaraza ya kata mara nyingi hukumbana na changamoto kadhaa, zikiwemo: Uelewa mdogo wa wananchi kuhusu taratibu za ardhi, na upungufu wa mafunzo kwa wajumbe wa mabaraza.

Changamoto nyingine ni ushawishi wa kisiasa na rushwa jambo linaloweza kuwafanya wajumbe kupendelea upande mmoja.

Kwa kupitia mafunzo hayo amesema mabaraza hayo yamefundishwa usuluhishi wa migogoro ya ardhi,  ukatili wa kijinsia na utawala bora.

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Iringa, Antigon John ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanaandika wosia ili kupunguza migogoro ya ardhi ndani ya familia.

Alieleza kuwa migogoro mingi inayofika katika mabaraza inahusiana na urithi wa ardhi, jambo ambalo linaweza kuepukwa kwa kupanga urithi mapema.

Amesema mabaraza mengi yamekuwa yakitoa maamuzi badala ya kusuluhisha, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linaweza kuwaumiza wananchi.

“Tunaamini semina hii imewapa uelewa mzuri wajumbe wa mabaraza haya, kwani wao ndio walioko karibu na wananchi. Baada ya mafunzo haya, tunatarajia kuona mabaraza yakitekeleza wajibu wake ipasavyo kwa kuzingatia sheria na kuimarisha usuluhishi wa migogoro ya ardhi,” amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments