Simba pumzi muhimu Misri


 KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema wataingia kwenye mchezo wa leo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Masry, Uwanja wa Suez Canal kwa lengo la kupata bao la ugenini.

Fadlu alisema anaamini mchezo wa marudiano utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Aprili 9 utaamua timu itakayoingia robo fainali, hivyo ni muhimu kwao kupata bao la ugenini kwenye mchezo wa leo.

“Naamini mchezo wa marudiano nyumbani utaamua timu itakayoingia robo fainali, hivyo malengo yangu kwenye mchezo wa leo ni kujaribu kupata bao la ugenini,” alisema Fadlu.

Alisema hana presha ya mchezo huo kwa sababu wamekuwa na rekodi nzuri za mechi za ugenini na kutolea mfano wa mechi dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya, CS Sfaxien na Maquis do Bravos ya Angola.

Hii ni robo fainali ya sita kwa Simba katika michuano ya CAF katika misimu saba kuanzia 2018/2019 na hakuna hata moja aliyovuka baada ya kushindwa kupata ushindi ugenini.

Katika robo zilizopita hii ni mara ya pili kuanzia ugenini na kutolewa mara mbili mfululizo kwa penalti dhidi ya Orlando Pirates (2021–2022) na Wydad (2022–2023) kwa ushindi wa penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa 1-1 mara zote.

Katika mchezo wa leo Simba itawakosa, Che Fondoh Malone ambaye ametoka kufanyiwa upasuaji hivi karibuni, Aishi Manula, Edwin Balua, Valentino Mashaka pamoja na Hussein Kazi kwa sababu za kiufundi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments