TANZANIA kwa kushirikiana na Namibia ipo katika mchakato wa kufanya ukarabati wa majengo ya kambi ya wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika ili itambuliwe na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama urithi wa dunia.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema hayo wakati wa ziara ya Rais wa Namibia, Nemtumbo Nandi-Ndaitwah katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Dar es Salaam jana.
Profesa Kabudi alisema sambamba na majengo hayo pia makaburi ya wapigania uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Namibia ambao wamezikwa nchini, yatakarabatiwa.
Alisema Tanzania ina historia ya kuwa nyumbani mwa wanaharakati waliopigania ukombozi katika nchi zao na waliishi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kongwa mkoani Dodoma.
Profesa Kabudi alisema Tanzania na Namibia ni nchi zenye historia inayofanana katika harakati za kujikomboa kutoka kwa wakoloni wa Kijerumani.
“Sisi wote ni waathirika wa ukoloni wa Wajerumani mauaji ambayo yalifanyika Namibia pia yalifanyika Tanzania kipindi cha Vita ya Majimaji ambapo zaidi ya Watanzania 200 waliuawa wakati wakipambana na ukoloni,” alisema.
Profesa Kabudi alisema kati ya mwaka 1964 na 1994 kituo hicho kilikuwa nyumbani kwa wanaharakati kutoka nchi za Afrika akiwemo Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Namibia, Sam Nujoma.
“Leo nyumba hii ni zaidi ya makumbusho, ni utambulisho wa Afrika na Fursa kwa kizazi cha sasa kufahamu mchango wake katika harakati za ukombozi zilizofanywa na viongozi,” alisema.
Aidha, Profesa Kabudi amemshukuru Rais Nemtumbo kwa kutembelea kituo hicho na kuahidi kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta za utamaduni, sanaa na michezo.
Amemkabidhi Rais Nemtumbo Kamusi ya Kiswahili kwa ajili kujisomea na kuimarisha uzungumzaji wake wa Kiswahili.
0 Comments