Katika mikutano hiyo, Mhe. Kimambo alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati yake, viongozi wa mitaa, wananchi na serikali kuu, huku akisisitiza kuwa miradi mingi iliyotekelezwa imelenga kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji safi na uboreshaji wa mazingira ya biashara.
"Tumetekeleza miradi kwa uwazi mkubwa na kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi. Tumejenga shule mpya, barabara za mitaa na tumeboresha huduma za kijamii ambazo zimeleta tija kubwa kwa wananchi wetu," alisema Diwani Kimambo huku akishangiliwa na wakazi wa mtaa wa Mji wa Zamani.
Katika mtaa wa Bomani, Mhe. Kimambo alitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na ujenzi wa darasa la kisasa katika shule ya msingi Mughanga, upanuzi wa zahanati ya kata kuwa kituo cha afya, ujenzi wa lami ya barabara ya Bomani–Mji wa Zamani, na usambazaji wa maji safi kupitia mradi wa maji wa jamii.
Wananchi waliopata fursa ya kuchangia walimpongeza Diwani Kimambo kwa kuwa kiongozi wa mfano aliyesimama na wananchi bega kwa bega, akihakikisha kila mtaa unapata maendeleo kwa usawa bila upendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bomani, alieleza kuwa maendeleo hayo yamebadilisha maisha ya wananchi na kuifanya kata ya Mughanga kuwa mfano wa kuigwa ndani ya Manispaa ya Singida.
Mikutano hiyo ilikuwa sehemu ya ziara maalum ya kutoa mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha 2020–2025, ikiwa ni maandalizi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Na Abdul Ramadhani Singida
0 Comments