Baraza la Maendeleo ya Kata (WDC) ya Kindai limempongeza kwa dhati Mheshimiwa Diwani Omary Salum Kinyeto kwa kuonesha ushirikiano wa hali ya juu na wananchi pamoja na viongozi wengine wa serikali katika kusukuma gurudumu la maendeleo ndani ya kata hiyo kwa kipindi cha miaka mitano (2020–2025).
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mwaka 2020 hadi 2025, Diwani Kinyeto ameonyesha uwajibikaji wa hali ya juu kwa kusimamia utekelezaji wa miradi zaidi ya 20 ya maendeleo inayogusa sekta muhimu kama elimu, miundombinu, afya, maji, mazingira na shughuli za kijamii.
Akizungumza kwa niaba ya WDC, Mtendaji wa Kata ya Kindai Bw. Hassan B. Ally alisema, “Mheshimiwa Diwani ameendelea kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na wananchi, wadau wa maendeleo na serikali kwa ujumla. Ushirikiano huu umetuletea mafanikio makubwa, ukiwemo ujenzi wa madarasa, ofisi za walimu, barabara, vyoo, na hata vifaa vya matumizi ya kijamii kama vile viti 135 vilivyonunuliwa kwa ajili ya huduma kwenye jamii.”
WDC imepongeza juhudi binafsi za Diwani Kinyeto katika kuhakikisha miradi haikwami, huku akitoa michango yake binafsi pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu. Pia, ushiriki wake katika ufuatiliaji wa mikopo ya vikundi vya wanawake na vijana umeongeza uaminifu na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za serikali na wadau.
Aidha, WDC imetaja mafanikio mengine yaliyochangiwa na diwani huyo kuwa ni pamoja na:
Kupandwa kwa miti zaidi ya 5,700 kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.
Ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami na vivuko katika mitaa mbalimbali.
Usimamizi wa miradi ya BOOST kwa ajili ya shule za msingi.
Utoaji wa elimu ya ujasiriamali kwa makundi ya vijana na wanawake kwa kushirikiana na mashirika kama Faraja Centre, Helvetas na Hand in Hand.
Katika pongezi zao, WDC imemwomba Mheshimiwa Diwani Kinyeto aendelee na moyo huo wa kujitolea na kuwa karibu na wananchi, kwa kuwa mchango wake umekuwa dira ya mafanikio ya Kindai katika miaka mitano iliyopita.
“Tumeona tofauti kubwa katika maendeleo ya kata yetu chini ya uongozi wake. Sisi kama WDC tunaahidi kuendelea kushirikiana naye na kuhakikisha Kindai inaendelea kusonga mbele,” ilisisitiza taarifa ya baraza hilo.
Matukio mbali mbali kwa Picha Katika kikao hicho.
Kindai, Singida 18– Juni 2025 na Abdul Ramadhani
0 Comments