
Yagi Kiaratu, mmoja wa viongozi wanaoaminiwa, kuheshimiwa na kupendwa ndani ya Manispaa ya Singida, ameendelea kuwa jina linalotajwa kwa matumaini makubwa ya mabadiliko chanya. Kiaratu si tu mwanasiasa mwenye uzoefu, bali ni mtumishi wa watu, mwenye historia ndefu ya mafanikio katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kiutawala.
Akiwa amewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi alijijengea sifa ya kuwa kiongozi wa vitendo. Alisimamia kwa mafanikio miradi ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa barabara za mijini, huduma za afya, elimu na miundombinu ya kijamii, huku akisisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika kila hatua ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Lakini uwezo wa Yagi haukuishia kwenye siasa tu. Kwa sasa, yeye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Singida (SWFA) — nafasi ambayo ameigeuza kuwa jukwaa la kuinua vipaji vya wasichana na kuimarisha michezo kama sehemu ya maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla. Mbali na hapo, Yagi pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), nafasi inayomuweka katika ulingo mpana wa kitaifa katika kukuza sekta ya michezo nchini.
Wengi humtambua kama mshiriki mzuri wa kazi mbalimbali za kijamii, ambaye hupatikana kirahisi katika shughuli za kijamii, matukio ya maendeleo na mikutano ya wananchi. Ukaribu wake na watu, usikivu na uwezo wa kusikiliza na kutatua kero kwa hekima, vimewafanya wengi kumuona kama kiongozi wa mfano katika kizazi hiki.
Katika mahojiano ya hivi karibuni, Kiaratu alisisitiza msimamo wake wa kuwatumikia wananchi kwa vitendo akisema:
“Uongozi ni dhamana. Tunapopewa nafasi hatupaswi kuhutubia watu kwa maneno matupu, bali kwa vitendo vyenye tija. Ndiyo falsafa yangu.”
Leo hii, wananchi wa Singida Mjini wana sababu ya kujivunia na kuwa na matumaini mapya. Wanaona ndani ya Yagi Kiaratu mtu mwenye maono, aliyebeba historia ya kweli ya mafanikio, uzoefu usiotiliwa shaka, na moyo wa dhati wa kuwatumikia bila ubaguzi.
Kwa wale wanaotamani Singida yenye dira, maendeleo na mshikamano wa kweli — Yagi Kiaratu7
ni mwanga wa matumaini mapya.



0 Comments