Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida Mjini, Lucia Mwilu, amewataka wapinzani kuacha tabia ya kufanya siasa za kiherehere zisizo na tija kwa wananchi, badala yake wajifunze kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeendelea kuaminika kutokana na utekelezaji wa Ilani yake.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Mughanga, Mwilu aliwanadi wagombea wa CCM akiwemo Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya urais, Yagi Kiaratu kwa ubunge, na Valeriani Kimambo kwa udiwani, ambapo aliwaeleza wananchi kuwa wagombea hao ndio chaguo sahihi la kuendelea kuwaletea maendeleo ya kweli.
“Wapinzani wanapiga kelele zisizo na msingi, wakijishughulisha na kiherehere cha kisiasa kama nywele, wakati wananchi wanataka kuona shule bora, barabara zinazopitika na huduma za afya zenye ubora. Ni CCM pekee iliyoonesha dira ya maendeleo kwa vitendo,” alisema Mwilu huku akishangiliwa na wananchi.
Alisisitiza kuwa kazi kubwa imefanywa katika kipindi cha uongozi wa CCM, kuanzia miradi ya maji, elimu, afya hadi miundombinu, na kuwataka wananchi wa Mughanga na Singida kwa ujumla kuendelea kuiamini CCM ili kuendeleza mafanikio hayo.
Kwa upande wao, wananchi waliohudhuria mkutano huo walionyesha imani kubwa kwa wagombea wa CCM na kuahidi kuwapa kura zote za kishindo ifikapo siku ya uchaguzi.





0 Comments