Wazazi CCM Singida Watangaza Mapambano ya Kura: “Kila Mmoja Atoke Aendeshe Harakati za Ushindi”

                                 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Singida, Bi. Bertha Nakomolwa, ameibua ari mpya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwataka viongozi na wanachama wote kusimama kidete kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.

Akizungumza leo wilayani Iramba katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa makundi mbalimbali ya kijamii, Bi. Nakomolwa alisisitiza kuwa huu si wakati wa kukaa kimya bali ni muda wa kila mmoja kutumia nafasi yake kusimama mstari wa mbele katika kutafuta kura.

“Kila mmoja wetu ana wajibu. Huu ni wakati wa kwenda kwa wananchi, kueleza mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya uongozi thabiti wa viongozi wetu. Ni wakati wa kuimarisha mshikamanon wa chama chetu na kushirikiana bega kwa bega kusaka ushindi wa kishindo,” alisema.

                                      Mara baada ya hotuba yake, Bi. Nakomolwa aliongoza matembezi ya miguu katika kata ya Kiomboi, akizungumza ana kwa ana na makundi mbalimbali ya wananchi. Katika ziara hiyo, aliendelea kufafanua utekelezaji wa sera za CCM na mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya, maji, na miundombinu, akisisitiza kuwa chama hicho kimejipambanua kama kinara wa maendeleo ya kweli.

                                     

Mbinu ya kuwakutanisha viongozi na wananchi uso kwa uso imeonekana kuibua matumaini mapya na kuongeza mshikamani kwa wanachama na wafuasi wa CCM. Bi. Nakomolwa alisisitiza kuwa kila kada wa chama anapaswa kuzungumza ukweli na kuonyesha ushahidi wa miradi iliyotekelezwa ili wananchi waone thamani ya kura zao.

                                      

“CCM tumetekeleza, tumethibitisha, na tutaendelea kusonga mbele. Ni wajibu wetu kushirikiana na wananchi kuhakikisha tunabaki kuwa chama kinachoaminika kwa vitendo na si maneno matupu,” aliongeza.

Kauli ya Bi. Nakomolwa imechochea msisimko mkubwa ndani ya jumuiya ya wazazi na wanachama wa CCM kwa ujumla, ikionekana kuwa mwito wa mapambano ya kisiasa kwa vitendo na si kwa maneno pekee.

Kwa namna alivyoendesha mkutano na kufuatilia kwa vitendo kupitia matembezi ya mtaa kwa mtaa, wananchi wengi walionyesha shauku kubwa na kuahidi kuendelea kuunga mkono sera za CCM, wakibainisha kwamba maendeleo yanayoonekana ni kielelezo cha uongozi makini wa chama hicho.

Alifu Abdul Singida, Iramba 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments