Akiwasili mkoani Singida, wilaya ya Ikungi, jimbo la Ikungi Magharibi, Hapi alifanya mkutano wa hadhara katika kitongoji cha Ifyamahumbi, kata ya Mtundulu, ambapo alihutubia mamia ya wananchi waliokusanyika kumsikiliza. Katika hotuba yake, alieleza kwa kina mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM, akibainisha kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa uongozi imara wa chama hicho na serikali yake.
Hapi pia hakusita kuwanadi wagombea wa CCM akiwemo Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Ubunge wa Ikungi Magharibi Mheshimiwa Kingu. Aliwataka wananchi kumchagua Kingu akimtaja kama kiongozi mcheshi, mchezeshaji na mwenye nafasi kubwa ya kuchochea maendeleo ya wananchi wa Ikungi na taifa kwa ujumla.
Akitoa wito mahsusi, Hapi aliwaomba wananchi wa Ikungi na Singida kwa ujumla kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu kwa kuwapigia kura wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya diwani, mbunge hadi urais.
Kwa msisitizo, Hapi alisema: “Ushindi wa CCM si ushindi wa chama pekee, bali ni ushindi wa wananchi wote wa Tanzania. Ni ushindi wa maendeleo, mshikamano na ustawi wa Taifa letu.”
Na Alifu Abdul Singida




0 Comments