KINDAI YASIMAMA IMARA — KINYETO AONGOZA UPEPO WA MAENDELEO, WANANCHI WAAHIDI KURA ZA KISHINDO KWA CCM

 Hali ya kisiasa katika Kata ya Kindai, Manispaa ya Singida, imezidi kupamba moto huku wananchi wakionyesha imani kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wagombea wake. Hayo yamejidhihirisha wazi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika Mtaa wa Mahembe, ambapo Mgombea Udiwani wa CCM, Comrade Omary Salumu Hamisi (Kinyeto), alipowasili akipokelewa kwa shangwe, nderemo na hamasa kubwa kutoka kwa wananchi.

Kauli maarufu iliyoibuka katika mkutano huo, “Wanakindai hatukudai!”, ilibeba ujumbe mzito wa kisiasa, ikiashiria imani ya wananchi kwamba hawakuhitaji maneno matupu bali wanamtaka kiongozi mwenye kazi, uadilifu na maono ya kweli ya maendeleo — sifa ambazo wanaziona kwa Comrade Kinyeto.

Akizungumza katika mkutano huo, Meneja wa Kampeni wa Kata ya Kindai, Comrade Hamisi Kitila, alisema wananchi wa Kindai wamejipanga vizuri kuhakikisha kuwa CCM inaibuka na ushindi wa kishindo katika ngazi zote za uongozi.

“Zimebaki siku nne tu, na sisi Kindai tumeamua. Tutampigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Urais, Mh. Yagi Maulidi Kiaratu kwa Ubunge wa Singida Mjini, na Comrade Omary Salumu Hamisi (Kinyeto) kwa Udiwani wa Kata yetu ya Kindai. Huu ndio wakati wa kazi, si maneno,” alisema Kitila huku akishangiliwa na wananchi.

Katika hotuba yake, Comrade Kinyeto aliwashukuru wananchi kwa imani waliyoionesha kwake, akisisitiza kuwa ushindi wa CCM katika Kata ya Kindai ni ushindi wa maendeleo ya watu.

“Ninachowaomba ni jambo moja tu — tutoke kwa wingi siku ya kupiga kura. Tuitikie wito wa amani, umoja na maendeleo. Kura zetu kwa CCM ndizo zitakazolinda miradi yetu na kuendeleza kazi nzuri ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema kwa msisitizo.

Wananchi wa Kindai wameendelea kuonyesha mshikamano mkubwa, huku hamasa ya kampeni ikionekana kila kona ya kata hiyo. Kwa kauli moja, wameamua kuandika historia mpya ya kisiasa kupitia kura zao — historia ya maendeleo, amani na utulivu chini ya CCM.

Abdul Ramadhani Singida.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments