Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kenani Laban Kihongosi, amesema chama hicho kimepiga hatua kubwa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ambapo katika kuadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa CCM, kitaanza rasmi ugawaji wa kadi za kielektroniki kwa wanachama wake awamu ya pili.
Kihongosi ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida, ikiwa ni siku ya pili ya ziara hiyo, aliposhiriki mkutano na wanachama wa Shina namba moja, lililopo Kata ya Kindai, Manispaa ya Singida.
Akizungumza na wanachama wa shina hilo, Kihongosi amesema utekelezaji wa mfumo wa kadi za kielektroniki ni sehemu ya mkakati mpana wa CCM wa kujijengea uwezo wa kisasa katika uendeshaji wa shughuli zake, sambamba na kuimarisha uwazi, usalama wa taarifa za wanachama na ufanisi wa kiutendaji.
“CCM inaendelea kujibadilisha kulingana na mahitaji ya wakati. Matumizi ya Tehama si anasa bali ni hitaji la lazima. Mfumo wa kadi za kielektroniki umeshakamilika na sasa tunaelekea awamu ya pili ya ugawaji wake,” amesema Kihongosi.
Ameeleza kuwa kadi hizo zitasaidia kutambua wanachama halali wa chama, kurahisisha usimamizi wa taarifa, pamoja na kuongeza uwajibikaji katika ngazi zote za uongozi wa chama kuanzia shina hadi Taifa.
Aidha, Kihongosi amewataka wanachama wa CCM kuendelea kukilinda chama chao kwa vitendo, kuimarisha mshikamano, nidhamu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama, huku wakitambua kuwa mageuzi ya kiteknolojia ni msingi muhimu wa kukiandaa chama kwa ushindani wa kisiasa wa sasa na baadaye.
Ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo mkoani Singida inalenga kukagua uhai wa chama mashina, kusikiliza maoni ya wanachama, kuimarisha itikadi ya CCM pamoja na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu ya chama katika ngazi za chini.
Na Bandola Media – Singida







0 Comments