Ni siku yenye mchanganyiko wa huzuni na shukrani kwa wadau wa soka mkoani Singida, baada ya Deus almaarufu Geme Chenger kuagwa rasmi leo kupitia mechi ya hisani iliyochezwa kati ya Singida Veterani na Vijana wao, kufuatia kupata uhamisho wa kikazi kutoka Singida kwenda Tabora.
Mechi hiyo haikuwa ya kawaida, bali ilikuwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa Deus “Geme Chenger” katika maendeleo ya michezo, hususan soka, ndani ya mkoa wa Singida. Wadau mbalimbali wa michezo, viongozi na mashabiki walijitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, Kocha Mkuu wa Singida Veterani, Edwini Hagai, alisema kuondoka kwa Deus ni pigo kubwa kwa wadau wa soka mkoani Singida, akisisitiza kuwa amekuwa nguzo muhimu siyo tu katika michezo, bali pia katika shughuli mbalimbali za kijamii.
“Deus Geme Chenger amekuwa mshiriki wa kweli katika maendeleo ya michezo Singida. Ametoa mchango wake kwa vitendo, moyo na muda wake. Kuondoka kwake ni pengo kubwa, lakini tunamshukuru kwa yote aliyoyafanya,” alisema Kocha Hagai.
Kocha huyo aliendelea kuwasisitiza wanachama wa Singida Veterani na wadau wa michezo kuiga mfano wa Deus, hasa kwa namna anavyojitolea bila kuchoka katika masuala ya kijamii na michezo, akieleza kuwa huo ndio msingi wa maendeleo ya kweli ya soka.
Licha ya kuondoka Singida, Deus Geme Chenger ameahidi kuendelea kuwa karibu na familia ya michezo ya Singida, akisisitiza kuwa Singida itaendelea kuwa nyumbani kwake milele.
Matukio Mbali Mbali Kwa Picha Katika Tukio Hilo.















0 Comments