Kihongosi vitendo zaidi ya maneno – Ambulance yaja kuokoa maisha Singida Vijijini.


Na Bandola Media – Singida
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Kenani Laban Kihongosi, ameagiza Wizara ya Afya kuhakikisha gari la wagonjwa (Ambulance) linafikishwa haraka katika Hospitali ya Wilaya ya Singida Vijijini, iliyopo Ilongero, ili kuboresha huduma za dharura kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Kihongosi alitoa agizo hilo leo Jumatatu Januari 19, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Singida. Mradi huo wa kimkakati unaogharimu Shilingi bilioni 3.7, unatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa wa huduma za afya kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Katika hatua ya kuonesha uwajibikaji wa haraka, Komredi Kihongosi alimpigia simu moja kwa moja Waziri wa Afya, Mhe. Mohamedy Mchengerwa, na kumuagiza wizara yake kuhakikisha gari hilo linafika kwa wakati ili hospitali iweze kutoa huduma kamili kama ilivyokusudiwa.

Amesisitiza kuwa uwepo wa ambulance ni jambo la msingi, hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo inahudumia tarafa tatu, ambapo wananchi wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri wa dharura kwa wagonjwa, hususan akina mama wajawazito, watoto na wagonjwa mahututi.
“Hatuna budi kuhakikisha miundombinu ya afya inakwenda sambamba na vifaa muhimu vya huduma. Hospitali bila ambulance ni sawa na huduma isiyokamilika,” alisisitiza Kihongosi.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na matumaini makubwa na wananchi wa Singida Vijijini, wakieleza kuwa itaondoa adha ya muda mrefu ya kusafirisha wagonjwa kwa gharama kubwa na umbali mrefu, na hivyo kuokoa maisha ya watu wengi.

Ziara ya Ndugu Kenani Kihongosi mkoani Singida inaendelea kuonesha uthubutu wa uongozi wa CCM katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na rasilimali za Taifa.












TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments