Yagi Kiaratu Akabidhi Hatima ya Singida Mjini kwa Wazee: Amani, Mila na Mustakabali wa Kizazi Kijacho”

Katika hatua inayoonesha uongozi wa busara, heshima na mshikamano wa kijamii, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Yagi Kiaratu, amekutana na wazee wa jimbo hilo katika kikao cha kihistoria kilicholenga kujadili masuala ya msingi yanayohusu mustakabali wa Singida Mjini, kwa kuzingatia maadili, mila na mabadiliko ya nyakati.

Kikao hicho kilikuwa jukwaa muhimu la kusikiliza hekima na uzoefu wa wazee, ambao ni hazina ya jamii, pamoja na kuweka mwelekeo wa pamoja wa maendeleo ya jimbo hilo. 

Akizungumza kwa unyenyekevu na heshima, Mbunge Kiaratu aliwashukuru wazee kwa kuendelea kumuamini na kusimama naye katika safari ya kuwatumikia wananchi wa Singida Mjini.
                                   

Mbunge huyo alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo yoyote ya kweli, akieleza kwa msisitizo kwamba amani ya Nchi yetu Tanzania  lazima ilindwe kwa gharama zozote. 

Alibainisha kuwa wazee walitoa mchango mkubwa wa nguvu, hekima na maamuzi magumu hadi kufikisha jamii katika hali ya utulivu iliyonayo leo, hivyo ni wajibu wa kizazi cha sasa kuilinda na kuirithisha amani hiyo kwa vizazi vijavyo.

Aidha, Mbunge  Kiaratu alihimiza jamii kuendelea kudumisha mila na tamaduni kwa misingi ya maadili mema, akieleza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila jamii kujitambua ilikotoka, ilipo sasa na mwelekeo wake wa baadaye.  Alisema mila na tamaduni ni dira ya maadili inayolinda mshikamano wa jamii na kuzuia mmomonyoko wa maadili.

Kwa upande wao, wazee wa Jimbo la Singida Mjini walimpokea Mbunge wao kwa bashasha, heshima na upendo mkubwa, wakionesha imani waliyonayo kwake kama kiongozi anayejali misingi ya jamii. 

                                
Walimpongeza kwa kutambua nafasi yao katika uongozi na kutoa ushauri wa busara, wakimtaka aendelee kukutana nao mara kwa mara, angalau kila baada ya miezi minne, ili kuendelea kujadili masuala ya maendeleo, amani na ustawi wa jimbo kwa maslahi mapana ya Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.

Katika baraka zao, wazee walieleza kuwa Singida Mjini ni kitovu na jicho la maendeleo ya Mkoa wa Singida, hivyo mshikamano kati ya viongozi, wazee na wananchi ni nguzo muhimu ya kuijenga Singida yenye maadili, umoja na maendeleo endelevu.
Na Abdul Bandola Singida

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments