KIEMI ANG’ARA KITAIFA: SERIKALI YAVUTIWA NA JUHUDI ZAKE KUINUA NA KULINDA MALI KALE KIJIJI CHA NYUKI KISAKI

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeonesha kuvutiwa kwa kiwango kikubwa na juhudi za Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Kijiji cha Nyuki Kisaki, Bw. Philemon Kiemi, kufuatia kazi yake ya kipekee katika kutambua, kulinda na kuendeleza maeneo ya mali kale yenye thamani ya kihistoria na kitamaduni.

Ziara ya Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mambo ya Kale Tanzania, Bw. Emmanuel Bwasili, katika kijiji hicho imekuwa ushuhuda wa mafanikio ya juhudi hizo, ambapo Serikali imejionea moja kwa moja hazina ya mali kale iliyopo pamoja na namna ambavyo imehifadhiwa kwa weledi mkubwa chini ya uongozi wa Kiemi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bw. Bwasili alimpongeza kwa dhati Bw. Kiemi, akimtaja kuwa ni mfano wa kuigwa katika juhudi za kizalendo za kulinda urithi wa taifa. Amesema dhamira, ubunifu na uthubutu wa Kiemi umeifanya Kijiji cha Nyuki kuwa kitovu muhimu cha utalii wa kiutamaduni na hifadhi ya historia hai ya Watanzania.

 Kiemi ameonesha uongozi wa mfano. Amechukua hatua madhubuti si tu kuhifadhi mazingira bali pia kuibua na kulinda mali kale ambazo leo zinatambulika kama fahari ya taifa na dunia. Huyu ni kiongozi mwenye maono makubwa,” amesema Bw. Bwasili.

Kwa miaka kadhaa sasa, Bw. Kiemi amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira na mali kale, akiamini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na kuthamini urithi wa asili. Kupitia juhudi zake, Kijiji cha Nyuki kimeendelea kung’ara kama mfano bora wa usimamizi wa rasilimali za kijamii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Serikali imewataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo kwa kuhakikisha maeneo ya mali kale yanaendelea kulindwa, huku ikisisitiza kuwa uwepo wa hazina hiyo ni fursa adhimu ya kukuza uchumi kupitia utalii, ajira na kuimarisha utambulisho wa taifa.

Kwa upande wake, Bw. Philemon Kiemi ameishukuru Serikali kwa kutambua kazi yake na kuahidi kuendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha Kijiji cha Nyuki kinakuwa kitovu cha mfano cha utunzaji wa mali kale na maendeleo endelevu.

Mali kale zilizopo Kijiji cha Nyuki Kisaki zimeendelea kutajwa kuwa ni alama muhimu ya historia na utamaduni wa Tanzania, huku juhudi za Bw. Kiemi zikichukuliwa kama chachu ya mageuzi katika sekta ya utalii wa kiutamaduni nchini.
Na Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments