SEKTA BINAFSI YAHAMASISHWA KUCHANGAMKIA MIRADI YA UBIA KUCHOCHEA MAENDELEO


WADAU  wa sekta binafsi wamehimizwa kutumia kikamilifu fursa za uwekezaji kupitia miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini. Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam katika mafunzo maalum yaliyolenga kuongeza uelewa na uwezo wa wadau kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Kituo cha PPP na Jukwaa la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), yamekuja wakati ambapo Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia maboresho ya sheria na miongozo ya ubia. Hatua hiyo inalenga kuvutia ushiriki mpana zaidi wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.

Washiriki walipata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu mfumo wa PPP, ikiwemo taratibu za kuibua, kuandaa na kutekeleza miradi, sambamba na namna ya kutathmini hatari na faida zake. Aidha, walielekezwa jinsi ya kutumia taarifa za orodha ya miradi (pipeline) ili kubaini maeneo yenye fursa za uwekezaji.

Kupitia majadiliano ya kitaalamu na uzoefu wa wataalam, ilibainika kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kusaidia Serikali kufanikisha malengo ya muda mrefu ya maendeleo, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Wadau walisisitizwa kuwa ubia si ubinafsishaji, bali ni ushirikiano unaolenga kuongeza ufanisi na tija.


Kwa ujumla, mafunzo hayo yameibua mwamko mpya kwa wadau wa sekta binafsi kuona umuhimu wa kushiriki katika miradi ya ubia, huku yakitoa mwanga wa namna bora ya kunufaika na fursa zilizopo na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments