KIJIJI CHA NYUKI CHAVUTA MAELFU YA WAFUGAJI NA WANUNUZI, PHILEMON KIEMI AENDELEA KUFUNGUA FURSA ZA UCHUMI WA ASALI TANZANIA

Katika hatua inayoendelea kuonesha mapinduzi makubwa ya sekta ya ufugaji nyuki nchini, zaidi ya wafugaji na wanunuzi 1,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamekusanyika katika Kijiji cha Nyuki kwa lengo la kupata elimu ya kisasa kuhusu ufugaji wa nyuki kibiashara, uchakataji wa mazao yatokanayo na nyuki pamoja na fursa za masoko ya uhakika.

Washiriki hao wamepata nafasi ya kujifunza kwa vitendo namna mazao mbalimbali yatokanayo na nyuki ikiwemo asali, nta, gundi ya nyuki na bidhaa nyingine zinavyozalishwa, kuchakatwa na kuandaliwa kwa viwango vya kisasa vinavyokidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, mwanzilishi na Mkurugenzi wa Kijiji cha Nyuki, Philemon Kiemi, amesema dhamira yao ni kuwabadilisha wafugaji nyuki kutoka ufugaji wa mazoea kwenda ufugaji wa kibiashara wenye tija na manufaa makubwa kiuchumi.

Amesema Kijiji cha Nyuki kimekuwa sehemu muhimu ya kuwajengea uwezo wafugaji kwa kuwapatia elimu ya kisasa, teknolojia rafiki pamoja na kuwaunganisha moja kwa moja na wanunuzi wa bidhaa za nyuki kutoka maeneo mbalimbali duniani.

“Lengo letu ni kuona mfugaji wa nyuki anakuwa na maisha bora kupitia bidhaa zake. Tunataka wafugaji wetu wawe na uhakika wa soko, bei nzuri na uelewa wa thamani ya mazao yao,” amesema Kiemi.

Mbali na elimu hiyo, washiriki walipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji na uchakataji wa bidhaa hizo, jambo lililowavutia wengi kutokana na ubora wa mifumo inayotumika pamoja na maandalizi ya kisasa yanayofanyika ndani ya Kijiji cha Nyuki.

Katika hali iliyoonyesha mafanikio makubwa ya programu hiyo, imeelezwa kuwa kila mfugaji na mnunuzi aliyeshiriki atapatiwa mkataba maalum wa biashara kulingana na mahitaji yake, hatua inayotajwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji wengi waliokuwa wakikosa masoko ya uhakika.

Washiriki kutoka mataifa mbalimbali wamepongeza juhudi za Philemon Kiemi wakieleza kuwa ameendelea kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya ufugaji nyuki Afrika Mashariki kwa kuunganisha elimu, biashara na teknolojia katika mfumo mmoja wenye manufaa kwa jamii.

Wengi wao wamekiri kuvutiwa na maono ya Kiemi ya kujenga uchumi kupitia sekta ya nyuki huku wakisema kuwa Kijiji cha Nyuki siyo tu kituo cha mafunzo, bali ni darasa kubwa la ujasiriamali na maendeleo ya wananchi.

Kupitia juhudi hizo, Kijiji cha Nyuki kinaendelea kuwa mfano wa kuigwa nchini Tanzania kwa namna kinavyowainua wafugaji wadogo, kuwafungulia masoko na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kwa kiwango cha kimataifa.

Sekta ya ufugaji nyuki imeendelea kuonekana kuwa miongoni mwa sekta zenye uwezo mkubwa wa kuongeza ajira, kukuza uchumi wa wananchi na kuiingizia taifa mapato kupitia bidhaa zinazohitajika kwa kiwango kikubwa duniani.







 Na Abdul Ramadhani Singida Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments