Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Moses Mlata, amewataka viongozi wa chama na serikali katika ngazi zote kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao badala ya kusubiri malalamiko yazidi kuongezeka.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kuimarisha chama pamoja na kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kukiamini na kukichagua Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Martha Mlata amesema CCM itaendelea kuwa chama cha matumaini kwa Watanzania kwa sababu kinaendelea kusikiliza na kutekeleza mahitaji ya wananchi wake.
Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Singida alisema kuwa dhamira ya chama hicho ni kuona wananchi wanapata huduma bora katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, afya, elimu, Kilimo miundombinu na maendeleo ya kiuchumi, huku akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa karibu na wananchi muda wote ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Viongozi lazima muwe sehemu ya suluhisho la changamoto za wananchi. Wananchi wametuamini na wametupa ridhaa ya kuendelea kuwaongoza, hivyo tunapaswa kuwatumikia kwa uadilifu, uwajibikaji na matokeo yanayoonekana,” alisema Martha Mlata.
Katika ziara hiyo, Martha Mlata ameendelea kuonyesha uwezo mkubwa wa kiuongozi na uthubutu wa kisiasa kwa kuhamasisha mshikamano, nidhamu na uwajibikaji ndani ya chama, huku akisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa nguzo imara ya maendeleo nchini kutokana na sera zake zinazolenga maslahi ya wananchi wa kawaida.
Aidha, amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Singida akiwa Wilani Manyoni kwa kuendelea kuiamini CCM na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, akieleza kuwa ushindi mkubwa wa chama hicho mwaka 2025 ni ishara ya imani kubwa waliyonayo wananchi kwa uongozi wa chama na serikali yake.
Wakazi na wanachama mbalimbali waliohudhuria ziara hiyo wilayani manyoni walieleza kufurahishwa na namna Mwenyekiti huyo anavyosimamia masuala ya chama kwa karibu, huku wengi wakimtaja kuwa ni kiongozi mwenye maono, msikivu na mwenye moyo wa kuwatumikia wananchi bila kuchoka.
Ziara ya Martha Mlata imeendelea kuacha alama kubwa ndani ya Manyoni na Mkoa wa Singida kwa ujumla na kuimarisha ari ya wanachama, kuongeza mshikamano wa chama pamoja na kuhamasisha kasi mpya ya utekelezaji wa maendeleo kwa wananchi.
Na Abdu Ramadhani Singida Tanzania

0 Comments