TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA MILIONI 167 KUPITIA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA NA USIMAMIZI WA MIRADI

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imefanikiwa kuokoa na kurejesha serikalini zaidi ya Shilingi Milioni 167 kupitia shughuli mbalimbali za ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato ya umma pamoja na uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sosthenes Kibwengo, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026 mbele ya waandishi wa habari.

Akizungumza katika taarifa hiyo, Kibwengo amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi kubwa za taasisi hiyo katika kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma pamoja na kuimarisha uwajibikaji katika taasisi za serikali na halmashauri mbalimbali mkoani Singida.

Kwa mujibu wa Kibwengo, zaidi ya Shilingi Milioni 56 zilirejeshwa serikalini baada ya TAKUKURU kufanya ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za kielektroniki za POS katika Halmashauri za Wilaya za Manyoni na Iramba. Uchunguzi huo ulibaini kuwepo kwa fedha ambazo hazikuwasilishwa benki kwa wakati kama inavyotakiwa kwa mujibu wa taratibu za ukusanyaji wa mapato ya umma.

Aidha, amesema zaidi ya Shilingi Milioni 76 zimerejeshwa kutokana na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi 28 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 8. Miradi hiyo ilihusisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji, barabara pamoja na utawala.

Kibwengo amesema TAKUKURU imeendelea kuhakikisha fedha za maendeleo zinatumika kwa ufanisi na kwa malengo yaliyokusudiwa ili wananchi waweze kunufaika na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Katika upande wa uchunguzi wa tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, TAKUKURU Mkoa wa Singida imefanikiwa kurejesha zaidi ya Shilingi Milioni 34 serikalini kupitia uchunguzi wa mashauri mbalimbali yaliyokuwa yakihusu matumizi mabaya ya fedha na mali za umma.

Kwa kipindi hicho, TAKUKURU ilipokea jumla ya malalamiko 95 kutoka kwa wananchi, ambapo malalamiko 51 yalihusu vitendo vya rushwa huku malalamiko 44 yakibainika kutohusiana na rushwa. Wahusika wa malalamiko hayo walipewa ushauri na maelekezo stahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Sambamba na hilo, mashauri sita ya jinai yalifunguliwa mahakamani katika kipindi hicho, huku mashauri matatu yakitolewa hukumu na Jamhuri kushinda mashauri yote matatu, jambo ambalo linaonesha uimara wa ushahidi na kazi ya uchunguzi inayofanywa na taasisi hiyo.

Kibwengo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma ili kuendelea kujenga jamii yenye uwazi, uwajibikaji na uadilifu.

Amesema katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2026, TAKUKURU Mkoa wa Singida imejipanga kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuongeza ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia makundi mbalimbali ya kijamii ili kujenga utamaduni wa kupinga na kuchukia rushwa.

TAKUKURU imeeleza kuwa ushirikiano wa wananchi ni silaha muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi pamoja na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.





Na Abdul Ramadhani Singida Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments