Serikali imeanza rasmi kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ya kushughulikia migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Singida, ikiwa ni siku chache baada ya maelekezo hayo kutolewa wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Ikungi na katika Manispaa ya Singida mnamo Juni 27, 2026.
Zoezi hilo limeanza kwa kikao maalumu kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, ambapo viongozi wa Mkoa, wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Timu ya Watalaamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wamekutana kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi iliyowasilishwa na wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa za viongozi wa mkoa, mamia ya wananchi walijitokeza na kuwasilisha migogoro yao pamoja na nyaraka na vielelezo mbalimbali vinavyohusiana na umiliki wa ardhi. Serikali imeeleza kuwa kila mwananchi atapewa nafasi ya kusikilizwa ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kuzingatia sheria, kanuni na ushahidi uliopo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, alimpongeza Kamishina wa Ardhi, Nathaniel Mathew Nhonge, kwa ushirikiano wake na kujitoa katika kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiathiri maendeleo ya wananchi katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo.
Zoezi hilo linatarajiwa kuendelea kwa siku nne, likiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wote waliojitokeza wanasikilizwa na kupata ufumbuzi wa changamoto zao kwa wakati.
Miongoni mwa viongozi wanaosimamia zoezi hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, Kamishina wa Ardhi, Nathaniel Mathew Nhonge, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe.
Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Serikali ya kusikiliza wananchi na kushughulikia migogoro ya ardhi kupitia utaratibu wa mazungumzo, usuluhishi na uamuzi unaozingatia sheria. Migogoro ya ardhi ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri uwekezaji, matumizi bora ya ardhi na maendeleo ya kijamii, hivyo utekelezaji wa maelekezo haya unatarajiwa kuchangia kuimarisha utulivu na maendeleo katika Mkoa wa Singida.
.jpeg)



0 Comments