MGONTO AIBUKA TENA IKUNGI, AWEKA WAZI NAMNA BAJETI YA 2026/2027 ITAKAVYOWAGUSA WANANCHI

                                     

Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti,Thomas Mgonto, ameendelea kuonyesha umahiri wake wa kuwasilisha masuala ya maendeleo kwa wananchi baada ya kueleza kwa kina manufaa ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/2027 katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, uliofanyika katika Viwanja vya Puma, Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.

Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi, Mgonto alisema bajeti hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuwagusa Watanzania wa kawaida, hususan wafanyabiashara wadogo, vijana, wanawake na wajasiriamali ambao ni mhimili muhimu wa uchumi wa nchi.

Alieleza kuwa moja ya maeneo muhimu yaliyoboreshwa ni mfuko wa mikopo unaotokana na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, ambapo Serikali imeelekeza kuongeza kiwango hicho hadi asilimia 15 kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa mikopo na kuweka mazingira bora zaidi kwa maendeleo ya wafanyabiashara na wajasiriamali.

Mgonto alisema hatua hiyo itaongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wengi zaidi, kuwasaidia kukuza biashara zao, kuongeza ajira na kuinua kipato cha familia.

Aidha, alieleza kuwa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 imeweka kipaumbele katika kupunguza baadhi ya tozo na kodi zilizokuwa zinalalamikiwa na wafanyabiashara, hatua ambayo itachochea mazingira bora ya biashara na kuongeza ushindani katika uchumi.

Akirejea mchango wake aliowahi kuutoa Bungeni, Mhe. Mgonto alisema Serikali imefanyia kazi baadhi ya mapendekezo yaliyolenga kumpunguzia mwananchi wa kawaida mzigo wa kodi, ikiwemo kuweka unafuu katika baadhi ya maeneo yanayohusu uingizaji na ununuzi wa magari.

Kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mgonto alisema anaelewa kwa undani changamoto zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara, hivyo anaamini maboresho yaliyofanyika yataongeza ari ya kufanya biashara, kukuza uwekezaji na kuongeza mapato ya wananchi pamoja na Taifa.

Katika hotuba yake, Mbunge huyo alimpongeza Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kutembelea Wilaya ya Ikungi na kuzungumza moja kwa moja na wananchi kuhusu utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Serikali.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo walipata fursa ya kusikia maelezo kuhusu mwelekeo wa bajeti na namna itakavyotekelezwa kwa lengo la kuboresha maisha yao.

Kwa ujumla,  Thomas Mgonto ameendelea kujijengea taswira ya kiongozi anayesisitiza maendeleo, anayefuatilia masuala ya wananchi na kutumia nafasi yake ya ubunge kueleza kwa uwazi sera na mipango ya Serikali kwa manufaa ya wananchi wa Ikungi Mashariki na Watanzania kwa ujumla.

Bajeti Yetu, Maendeleo Yetu.

Singida  Chemi ya Amani, Mshikamano na Maendeleo Endelevu.

Na Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments