Rais Samia Kutoa Tuzo Maalum kwa Walipakodi Bora Wakati TRA Ikiadhimisha Miaka 30

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inajiandaa kuandika historia mpya Julai 1, 2026 kwa kuadhimisha miaka 30 tangu kuanza rasmi shughuli zake, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuongoza hafla ya utoaji wa Tuzo Maalum za Rais kwa Walipakodi Bora wa mwaka wa fedha 2024/2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, Richard Kayombo, amesema maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Miongo Mitatu ya TRA, Mlipakodi Shujaa, Tanzania Inayojitegemea

Amesema maadhimisho hayo yatakuwa fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 30 ya utendaji wa TRA pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika ulipaji kodi kwa hiari, ambao ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa Kayombo, shughuli mbalimbali za kitaifa na kikanda zitaanza kabla ya kilele cha maadhimisho hayo Julai 1, 2026. Shughuli hizo zinalenga kuongeza uelewa wa masuala ya kodi, kuboresha huduma kwa walipakodi na kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa ni pamoja na vipindi maalum vya elimu ya kodi kupitia redio, televisheni na majukwaa ya kidijitali, kliniki za kodi, huduma za ushauri kwa walipakodi, mikutano na wadau mbalimbali wa sekta ya kodi pamoja na ziara maalum za kuwafikia walipakodi katika maeneo tofauti nchini.

Kayombo ameeleza kuwa maadhimisho hayo pia yataambatana na utoaji wa Tuzo Maalum za Rais kwa Walipakodi Bora, ambazo zinalenga kutambua na kuthamini mchango wa walipakodi walioonyesha uadilifu, uwajibikaji na uzalendo katika kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha utamaduni wa ulipaji kodi nchini na kuhamasisha wananchi zaidi kushiriki katika kujenga uchumi wa taifa kupitia mchango wao wa kodi.

“Malipo ya kodi si wajibu wa kisheria pekee, bali ni ishara ya uzalendo na ushiriki wa moja kwa moja katika maendeleo ya nchi. Kodi zinazokusanywa huchangia kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha miundombinu na kuleta fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi,” amesisitiza Kayombo.

TRA ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge mwaka 1995 na kuanza rasmi shughuli zake Julai 1, 1996. Tangu wakati huo, imeendelea kuwa taasisi muhimu katika usimamizi wa ukusanyaji wa kodi na mapato mengine ya Serikali Kuu, pamoja na kuweka mazingira yanayowezesha ulipaji kodi kwa hiari.

Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, TRA imepitia mageuzi mbalimbali ya kiutendaji na kiteknolojia yaliyolenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, kurahisisha utoaji wa huduma kwa walipakodi na kuimarisha uwazi katika mifumo ya kodi.

Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwake, kujadili changamoto zilizopo na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha mchango wa kodi katika kufanikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.

Kupitia maadhimisho hayo, TRA inalenga kuendelea kujenga uhusiano imara na walipakodi, kuimarisha uelewa wa masuala ya kodi na kuhamasisha ushiriki mkubwa zaidi wa wananchi katika safari ya kujenga Tanzania yenye uchumi imara na inayojitegemea.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments