TRA Iringa Yazindua Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mlipakodi na Miaka 30 ya Mamlaka

IRINGA: Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa imezindua ratiba ya shughuli zitakazofanyika kuanzia Juni 22 hadi 27, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mlipakodi kwa mwaka wa kodi 2024/2025 pamoja na kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.


Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Maigloria Saria, alisema maadhimisho hayo yanalenga kuimarisha uhusiano kati ya TRA na walipakodi, kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kodi na kutambua mchango wa walipakodi katika maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, shughuli za maadhimisho zitaanza Juni 22 kwa zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Tukio hilo linatarajiwa kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta.

Saria alisema Juni 23 kutafanyika jukwaa la wadau litakalowakutanisha wafanyabiashara, washauri wa kodi, viongozi wa dini na viongozi wa kimila. Jukwaa hilo litatoa nafasi ya utoaji wa elimu ya kodi, kupokea maoni kutoka kwa wadau na kujadili njia za kuboresha huduma zinazotolewa na TRA.

Aidha, Juni 24 na 26, maafisa wa TRA watatembelea maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuwashukuru walipakodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari, ambao ni msingi muhimu wa ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Katika mwendelezo wa shughuli hizo, Juni 25 TRA itatekeleza programu ya kurudisha kwa jamii kwa kutembelea wodi za wanawake na watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Siku hiyo pia Mkurugenzi wa Fedha wa TRA anatarajiwa kushiriki kipindi maalumu cha redio kitakacholenga kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kodi na mchango wake katika maendeleo ya taifa.

Maadhimisho hayo yatahitimishwa Juni 27 kwa matembezi ya hisani (Fun Walk) pamoja na msafara wa uelimishaji wa masuala ya kodi (Roadshow), utakaowashirikisha watumishi wa TRA, wafanyabiashara na wadau wengine. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Elimu ya Kodi Yapewa Kipaumbele
Akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo, Saria alisema yanaendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakumbusha wananchi wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, kutunza kumbukumbu sahihi za biashara na kushirikiana na mamlaka za kodi katika kutekeleza sheria za nchi.

Alibainisha kuwa moja ya changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa baadhi ya walipakodi ni uelewa mdogo wa masuala ya kodi. Kutokana na hali hiyo, TRA imeendelea kuwekeza katika programu mbalimbali za elimu kwa umma ili kuongeza uelewa na kuimarisha uzingatiaji wa sheria za kodi.

Kilele cha Kitaifa Julai 1
Saria alisema kilele cha Siku ya Mlipakodi kitaifa kitafanyika Julai 1, 2026. Baada ya maadhimisho hayo ya kitaifa, kila mkoa wa kikodi utaandaa hafla maalumu za kutambua na kuwapongeza walipakodi bora kwa kuwapatia vyeti na zawadi kutokana na mchango wao katika mwaka wa kodi 2024/2025.

Alitoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kuendelea kutimiza wajibu wao wa kikodi kwa hiari, akisisitiza kuwa mapato ya kodi yana mchango mkubwa katika kugharamia huduma za kijamii na miradi ya maendeleo nchini.

Ushirikiano wa walipakodi na TRA ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa. Tunawahimiza wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati ili kuchangia ustawi wa nchi yetu,” alisema Saria.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments