WAZIRI MKUU: HATUPASWI KUPUUZIA VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuwa walinzi wa amani na usalama wa Taifa kwa kutopuuza viashiria vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Akizungumza   Juni 28, 2026, katika ibada maalumu ya kilele cha harambee iliyofanyika Usharika wa Amani wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati, mjini Singida, Dkt. Mwigulu alisema kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania.

"Tuendelee kuhimizana kuhusu suala la ulinzi wa Taifa letu. Ulinzi wa Taifa letu ni wa kila Mtanzania na amani yetu ni ya kila Mtanzania," alisema.

Alisisitiza kuwa katika kipindi hiki, wananchi wanapaswa kuwa makini na kutoruhusu viashiria vya uvunjifu wa amani kupuuzwa, kwani vinaweza kuathiri maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.

"Sasa hivi hatupaswi kupuuzia viashiria vya uvunjifu wa amani hapa nchini. Hatutakiwi kuvipuuza kwa sababu vimetuachia doa," aliongeza.

Dkt. Mwigulu alieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo katika sekta zote, ikiwemo elimu, afya, biashara, uwekezaji na kilimo. Alibainisha kuwa mazingira yenye utulivu huwapa wananchi nafasi ya kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa uhuru na kuendelea kujenga uchumi imara.

Aidha, aliwataka viongozi wa dini, viongozi wa jamii na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhubiri mshikamano, upendo na uzalendo ili kudumisha umoja wa Watanzania. Alisisitiza kuwa tofauti za kisiasa, kijamii au kiimani hazipaswi kuwa chanzo cha migawanyiko inayoweza kuhatarisha amani ya Taifa.

Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda tunu ya amani ambayo Tanzania imeijenga kwa miaka mingi, huku ikiwataka wananchi kushirikiana na mamlaka husika kutoa taarifa za mapema kuhusu vitendo au mienendo inayoweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Amani ni msingi wa maendeleo. Kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda, kuitetea na kuirithisha kwa vizazi vijavyo.

Na Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments