Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Jesca Lebba, ametoa maelekezo kwa watumishi wa afya wa Hospitali ya Wilaya ya Iramba kuhakikisha wanaongeza kasi ya utekelezaji wa Sera ya Bima ya Afya kwa Wote kupitia usajili wa wananchi wengi zaidi, ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Dkt. Lebba ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya pamoja na kufanya kikao na Timu ya Usimamizi wa Huduma za Afya ya Halmashauri (CHMT).
Akizungumza na watumishi wa afya, Dkt. Lebba amesema Mkoa wa Singida umefikia asilimia 47 ya utekelezaji katika awamu ya kwanza ya usajili wa Bima ya Afya kwa Wote, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya watoa huduma za afya na maafisa wa bima ili kuongeza idadi ya wananchi wanaojiunga na mfumo huo.
"Kwa awamu hii ya kwanza, kama mkoa tupo asilimia 47. Twendeni tukashirikiane na wenzetu wa bima ya afya ili kuwasajili wananchi wengi zaidi," amesema Dkt. Lebba.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya sera hiyo yatategemea ushirikiano wa watumishi wa afya katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kuwa na bima ya afya, hatua itakayochochea upatikanaji wa huduma za afya kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dkt. Peter Luhenga, amewahimiza watumishi wa hospitali hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazokidhi viwango vya kitaifa.
Amesema utoaji wa huduma bora za afya ni msingi muhimu wa kujenga jamii yenye afya njema, kuongeza nguvu kazi ya taifa na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa takwimu za hospitali hiyo, Hospitali ya Wilaya ya Iramba ina uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja na kutoa huduma kwa takribani wagonjwa 325,000 kwa mwaka. Hospitali hiyo hutoa huduma mbalimbali za kibingwa na kibobezi zikiwemo tiba ya meno, huduma za afya ya uzazi na mama na mtoto, tiba mazoezi (Physiotherapy), upasuaji mkubwa na mdogo, huduma za maabara pamoja na huduma ya hewa tiba (Medical Oxygen).
Ziara ya Dkt. Lebba inaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya afya kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwamba utekelezaji wa Sera ya Bima ya Afya kwa Wote unafikia malengo yaliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya na kuimarisha ustawi wa jamii.
Na Abdul Ramadhani Tanzania













0 Comments