Chato, Geita. Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, amepongeza jitihada za vijana waliowekeza zaidi ya Shilingi bilioni 4.8 katika ujenzi wa kituo cha kisasa cha uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini cha TAMPMED Mining Ltd kilichopo Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita, akieleza kuwa uwekezaji huo ni mfano wa mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini.
Mhe. Mavunde alitoa kauli hiyo alipotembelea kituo hicho kwa lengo la kujionea maendeleo ya uwekezaji na uwezo wa teknolojia inayotumika katika kuongeza thamani ya madini ya dhahabu kabla hayajafikishwa sokoni.
Kituo cha TAMPMED Mining Ltd kinatoa huduma mbalimbali za kisasa katika sekta ya madini, ikiwemo uchenjuaji wa madini kwa teknolojia ya Carbon-in-Pulp (CIP), huduma za Elution, uchunguzi wa maabara kwa sampuli za madini pamoja na usambazaji wa kemikali zinazotumika katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo, kituo hicho kwa sasa kina plant tatu zenye uwezo wa kuchakata jumla ya tani 750 za udongo wa madini kwa mzunguko wa uzalishaji, huku shughuli za Vat Leaching zikiwa tayari zimeanza, hatua inayoongeza uwezo wa uzalishaji na ufanisi wa uchakataji wa madini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMPMED Mining Ltd, Bw. Ramadhani Tampela, alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika uwekezaji huo, kampuni bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya uchimbaji kutokana na ucheleweshaji wa ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye leseni za kampuni.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mchakato wa fidia kutaiwezesha kampuni kuendelea na shughuli za uchimbaji kwa ufanisi zaidi na kuongeza uzalishaji, huku akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa hauwezi kuzaa matokeo yaliyokusudiwa bila kuwa na maeneo ya kutosha ya uchimbaji wa madini.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mavunde alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wenye nia ya dhati ya kuendeleza sekta ya madini.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kupitia na kufuta leseni za uchimbaji zinazoshikiliwa na watu au taasisi ambazo hazijaendeleza shughuli za uchimbaji kwa muda mrefu, ili maeneo hayo yatolewe kwa wawekezaji wenye uwezo na dhamira ya kuwekeza na kuzalisha.
Mhe. Mavunde alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali za madini, kuhamasisha uwekezaji wa ndani, kuongeza ajira kwa vijana, kukuza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia sekta ya madini.
Ziara hiyo imeonyesha nafasi kubwa ya uwekezaji wa vijana wa Kitanzania katika kuendeleza teknolojia za kisasa za uongezaji thamani wa madini, hatua inayotarajiwa kuongeza ushindani wa sekta ya madini na kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

0 Comments