Hati Safi Yaiweka Singida Manispaa Kwenye Ramani ya Uwajibikaji, Yagi Kiarutu Atoa Salamu za Pongezi

                            

Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Yagi Maulid Kiaratu, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa kufanikiwa kupata Hati Safi katika ukaguzi wa hesabu za Serikali, akieleza kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho wa usimamizi mzuri wa fedha za umma, uwajibikaji na uongozi wenye matokeo.

Kiarutu alitoa pongezi hizo wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, leo Julai 04,2026 uliolenga kujadili taarifa na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumza mbele ya viongozi na watendaji wa Halmashauri na mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego , Mbunge huyo alisema kuwa kupata Hati Safi ni mafanikio yanayotokana na ushirikiano kati ya madiwani, wataalamu na watumishi wa Halmashauri katika kuhakikisha fedha za wananchi zinasimamiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Serikali.

Alisisitiza kuwa taarifa za CAG hazipaswi kuonekana kama nyaraka za ukosoaji pekee, bali ni mwongozo muhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na kuongeza tija katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kiaratu pia alitoa rai kwa viongozi na watumishi kuendelea kutekeleza mapendekezo ya CAG kwa wakati ili kudumisha rekodi nzuri ya Manispaa ya Singida na kuongeza imani ya wananchi katika matumizi ya rasilimali za umma.

“Niipongeze Manispaa Chini ya Mheshimiwa Mstahiki Meya kwa kupata hati safi lakini pia Niwapongeze kwa namna ambavyo mmeshughulika na hoja hizi Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Hoja za CAG zinatuonyesha ni namna gani tunafuata taratibu namna gani Tunafuata sheria na miangozo Mbalimbali,hizi hoja 46 tulizoletewa maana yake kuna mahali tumekosea ninawashukuru mmefuta hoja 30 mmebakisha hoja 16 ambapo pia mkuu wa Mkoa amesaidia na tukikaa vizuri tutazifuta zote”

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, mafanikio ya kupata Hati Safi yanaakisi dhamira ya Serikali ya kuboresha utawala bora, uwazi na uwajibikaji, huku yakitoa msingi imara wa kuendelea kuharakisha maendeleo ya miundombinu, elimu, afya na huduma nyingine muhimu kwa wananchi wa Singida Mjini.

Kupata Hati Safi ni zaidi ya mafanikio ya kiuhasibu; ni ishara ya taasisi inayoweka mbele maslahi ya wananchi kupitia matumizi sahihi ya fedha za umma.  Yagi Maulid Kiarutu ameendelea kuonyesha mshikamano wake na juhudi za maendeleo kwa kuhamasisha uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali za Serikali kwa manufaa ya wananchi wa Singida Mjini.
Na Abdul Ramadhani Tanzania

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560

Post a Comment

0 Comments